Waziri mkuu Vietnam kutua Tanzania na wawekezaji

Muktasari:

  • Balozi wa Vietnam nchini Tanzania, Nguyen Doanh amemweleza Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kuwa wafanyabiashara wasiopungua 20 wataongozana na naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Trinh Dinh Dung anayetarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania kati ya Julai 9 hadi 11, 2019.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania,  Kassim Majaliwa amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Vietnam kwa ajili ya kuwekeza katika sekta ya viwanda vinavyotumia malighafi za mazao ya kilimo.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumatano Julai 3, 2019 katika mazungumzo na balozi  wa Vietnam nchini Tanzania, Nguyen Doanh.

“Serikali imeendelea kuondoa  vikwazo vya  kuanzisha na kuendesha biashara  kwa kupitia upya sheria, kanuni na taratibu za biashara  na kuzifuta zile zilizothibitika kuyafanya mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kuwa magumu,” amesema Majaliwa.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Doanh amemweleza Majaliwa kuwa wafanyabiashara wasiopungua 20 wataongozana na naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Trinh Dinh Dung anayetarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania kati ya Julai 9 hadi 11, 2019.

Katika mazungumzo hayo, Majaliwa amemueleza  balozi huyo kuwa tayari Rais John Magufuli ameshaanzisha Wizara ya Uwekezaji iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuifanya Tanzania kuwa mahali bora na salama kwa wawekezaji na wafanyabiashara.