UCHOKOZI WA EDO: Waziri wa mambo ya ‘news’ ameniacha hoi

Nchi hii bwana. Kuna vitu ni ngumu kuacha vipite. Waziri wangu wa habari juzi akajibu swali fulani bungeni.

Namuheshimu sana. aliulizwa kuhusu mwandishi aliyepotea kiajabuajabu miaka miwili iliyopita, Azory Gwanda.

Waziri akang’aka. “Sitaki kuzungumzia kesi hii dhaifu. Hilo eneo ambalo amepotea kuna watu wengi wamepotea. Yeye huyo ndiye ambaye mnamuona dhahabu”. Nikatabasamu. Kwanza kwa kujikumbusha taaluma yake. Wanasheria ni watu makini. Nikajiuliza maswali mengi.

Ni kweli kupotea kwa mtu yeyote ni tatizo, hasa kama hajulikani alipo. Awe waziri, mkulima, mwandishi au kibaka bado linabakia kuwa tatizo kama akipotea. Hakuna kesi dhaifu katika kupotea mwanadamu. Lakini hapo hapo kuhoji kupotea kwa mtu mmoja hakuharamishwi na kupotea watu wengine.

Kwa mfano, kama mtu aliyepotewa na ndugu yake maeneo hayo aking’aka kuuliza alipo ndugu yake huwezi kumjibu kwa kusema ‘mbona kuna mwandishi amepotea eneo hilo na watu wameacha kumuulizia, ndugu yako ni nani hasa?’

Baadaye nikacheka kidogo nilipojikumbusha nafasi zetu katika jamii. Kuna watu wakipotea au wakiumwa inakuwa tofauti kidogo ingawa Mungu hapendi.

Kwa mfano, waziri mwenyewe aliwahi kupata matatizo ya kiafya katika utawala uliopita.

Tuliambatana naye kihisia pengine kuliko wagonjwa wengine waliokuwa hoi juu ya vitanda vya hospitali mbalimbali duniani.

Leo tungeandika ‘…apelekwa kwa matibabu India’. Kesho tungeandika ‘..apata nafuu’. Keshokutwa tungeandika ‘…kurejea kesho’. Wakati haya yanaandikwa sio kwamba kulikuwa hakuna wagonjwa wengine. Wanadamu bwana tunasahau sana.

Pia, mheshimiwa ametumia neno ‘dhaifu’ ambalo siku chache tu zilizopita limezua kasheshe pale mjengoni Dodoma. Huu ni usahaulifu mwingine.

Juzi tu jamani tulikuwa tunalipiga vita hili neno! Kulitumia tena katika jengo lilelile ni kitu cha kushangaza kidogo.

Maswali mengine pale Dodoma tuwe tunayajibu kwa hekima kidogo. Yanagusa jamii. Yanagusa baadhi ya familia za watu. Yasijibiwe kwa haraka bila ya kutafakari.

Kwa sasa akili yangu ipo Malawi kufuatilia ziara ya Namba Moja. Mara nyingi Namba moja akitembelea hizi nchi jirani watu wa huko hutetemeka. Wanajua chuma kimetua katika ardhi yao.

Haya ya mjengoni tunalazimika tu kuandika kwa sababu wakati mwingine ‘tunalazimishwa’.