Wema Sepetu alikoroga tena, aitwa kujieleza Bodi ya Filamu

Muktasari:

Wema alitangaza filamu hiyo jana katika ukurasa wake kwenye mtandao wa Instagram, filamu ambayo kacheza na Aunt Ezekiel wakiwa kama wahusika wakuu.

Bodi ya filamu imesema alichokifanya Wema Sepetu kutangaza filamu ya ‘Saa Mbovu’ sio sahihi kwa kuwa bado hawajamfungulia kujishughulisha na kazi za filamu.

Wema alitangaza filamu hiyo jana katika ukurasa wake kwenye mtandao wa Instagram, filamu ambayo kacheza na Aunt Ezekiel wakiwa kama wahusika wakuu.

Akizungumza jana na gazeti hili, Katibu Mtendaji wa Bodi hiyo, Joyce Fisoo, alisema wamesikitishwa na kitendo hicho na tayari wamemuita kumhoji kwa nini amefanya hivyo na kwa nini asichukuliwe hatua.

Alisema kanuni za sheria ya filamu na michezo ya kuigiza namba 156 za Mei 2011, kifungu cha 50 kinaeleza kuwa kwa yeyote atakayetenda kosa kwa kukiuka masharti ya kanuni hizo atatozwa faini isiyopungua Sh5 milioni.

Alibainisha kuwa mbali na kumuita Wema, pia walikihoji kituo cha Azam kujua kwamba wao ndio walimpa kazi ya kutangaza filamu hiyo, ambao walikana na kudai kuwa wanatangaza kupitia mitandao yao.

Kuhusu kumalizika kwa adhabu yake, alisema bado yupo katika uangalizi hadi Aprili mwakani, ambapo amepewa kazi tatu kubwa za kufanya na endapo wataridhika watatangaza kwa umma ni hatua gani watazichukua dhidi yake.

Alizitaja kazi hizo kuwa ni pamoja na kuandika maelezo ya maneno 1500 yakielezea mambo mazuri aliyowahi kuyafanya katika maisha yake.

Masharti mengine Fisoo amesema mshindi huyo wa tuzo za filamu za Azam ni kuandika maelezo mengine tena 1,500 ya changamoto alizokutana nazo katika maisha na namna gani anakusudia kurudisha taswira yake nzuri kwenye jamii ambayo imeharibika kwa sasa .

Wakati jambo la tatu, amesema anatakiwa kukutana na makundi yasiyopungua 500 na kuyaelezea hadithi yake na mambo gani mazuri watarajie kuyapata kutokana kwake huko aendako ambapo ndio wengi wanamsubiria kumuona kama atakuwa amebadilika kitabia.

“Katika kukutana na makundi haya anapaswa kutumia gharama zake na wala hatutamchagulia aina ya makundi lakini muhimu la kufanya katika sharti hili ni kuwasajili katika daftari na kutuletea muhtasari wa kile atakachokuwa amezungumza nao na maswali atakayokuwa ameulizwa.

“ Kazi zote hizo anapaswa kuzitimiza ndani ya miezi sita tangu wiki ya pili baada ya kuanza kutumikia adhabu yake na mpaka sasa kashaanza kutekeleza sharti la kwanza,” alisema Fisoo.