Wengi wamlilia Mengi, waeleza mchango wake kwa Taifa

Muktasari:

  • Watu wa kada mbalimbali wametumia mitandao ya kijamii kueleza mchango wa mwenyekiti mtendaji wa IPP, Reginald Mengi aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo akiwa Dubai

Dar es Salaam. Watu wa kada mbalimbali wametumia mitandao ya kijamii kueleza mchango wa mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo akiwa Dubai.

Wengi wamesema ni kati ya wafanyabiashara waliokuwa na upendo na walioacha alama itakayokumbukwa katika jamii.

Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mengi.

“Kama alivyopata kusema yeye mwenyewe siku za uhai wake kuwa watu wanaoacha alama hawafi, basi mawazo, falsafa, ubunifu na kujitoa kwake vitaendelea kuishi nasi,” amesema Dk Abbas.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema, “Pole kwa Jacqueline na Regina, Abdiel,  pacha na familia nzima ya IPP Group. Mungu ailaze roho ya Mzee Reginald Mengi peponi.”

Msanii Nandy kupitia ukurasa wake wa Instagram ameandika, “Pole sana wanafamilia, polee sana R.I.P mzee wetu.”

Msanii Mahsin Awadh maarufu Dk Cheni kupitia ukurasa wa Instagram ameandika, “R.I.P mzee wetu Mengi kweli kifo ni cha wote uwe na mali uwe masikini wote tutalala sehemu moja Mungu akupe pumziko la amani. Tangulia nasi tunakufuata pole sana”.

Yericko Nyerere kupitia Twitte ameandika, “Kazi zako hapa duniani hazina mfano, umeacha alama kubwa... Uende salama Mzee.”

Maria Sarungi amemtakia pumziko la amani na kueleza kuwa ametoa mchango mkubwa katika kukuza sekta ya viwanda nchini.

“ Pumzika kwa amani na Mungu awape faraja wanafamilia na marafiki katika kipindi hiki kigumu,” ameandika.

Waziri wa zamani wa maliasili na utalii, Lazaro Nyalandu kupitia ukurasa wake wa Twitter ameandika, “Poleni sana wana familia, ndugu, jamaa, na marafiki wa @regmengi kufuatia kuondokewa na mpendwa wetu, Reginald Mengi. Hakika, siku za maisha yetu zimehesabiwa na kuandikwa kitabuni. Ameimaliza safari yake hapa duniani. Iwe HERI kwake huko ng'ambo ya mto. RIP baba yetu.”

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye kupitia ukurasa wake wa Twitter ameadika, ““Umeacha alama kubwa! Nimejifunza mengi kwako, rafiki, mshikaji, kiongozi na mzazi! Ulinifundisha kuwa KUKATA TAMAA NI DHAMBI!, Msalimie Mzee Sitta, mkumbushe kile kikao chetu cha mwisho nyumbani kwako. Pumzika kwa amani Dr. R.A Mengi.”