Wenye kipato kidogo Dar wanavyotoka jasho mara 15 kununua maji ya Dawasa

Sunday January 06 2019
pic kipato

Wakazi wa Madale Kisauke, Dar es Salaam wakichota maji ambapo eneo hilo linakabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji ya bomba, hutoka mara 2 kwa Mwezi. Picha na Ericky Boniphace

Dar es Salaam. Wakazi wa Dar es Salaam ambao hawajaunganishwa kwenye mfumo wa majisafi wanalipa mara 15 zaidi ya waliounganishwa kununua uniti moja ya majisafi kutoka Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (Dawasa), Mwananchi limebaini.

Uniti moja ni sawa na lita 1,000.

Hali hiyo inawaumiza zaidi watu wenye kipato cha chini wanaolazimika kulipa kati ya Sh5,000 na Sh25,000 kununua kiasi hicho cha maji ya Dawasa kwa wanaotembeza kwa mikokoteni au wanaochota kwa waliounganishiwa huduma hiyo.

Ingawa uniti moja ya maji ya Dawasa inauzwa Sh1,663 kwa kila mkazi wa jiji aliyeunganishiwa, ni wazi kuwa wanaofaidi zaidi unafuu huo ni watu wenye kipato cha juu waishio maeneo ya Oysterbay, Masaki, Mbezi Beach, Kariakoo, Upanga, Posta na kwingineko ambako miundombinu ya majisafi imefika.

Wakazi wa maeneo ya Tandale, Buguruni, Gongo la Mboto, Manzese, Mbagala na maeneo mengine wanayoishi watu wa kipato cha chini hulipa kati ya Sh200 na Sh500 kununua ndoo moja ya lita 20 ya majisafi ya Dawasa.

Uchunguzi wa Mwananchi unaonyesha pia kuwa watu wanaoishi maeneo ya nje ya jiji kama Goba, Madale, Tegeta na baadhi ya maeneo ya Mbezi Beach ambao hawajaunganishwa kwenye mfumo wa majisafi hulipa kati ya Sh10,000 na Sh15,000 kununua uniti moja ya majisafi ya Dawasa.

Advertisement

Wananchi wanasemaje?

Familia ya Hajji Yusuph mwenye watoto sita na wajukuu wanane inayoishi Temeke kwa Azizi Ali ni kielelezo halisi cha jinsi watu wa kipato cha chini wanavyolipa gharama kubwa kununua majisafi.

“Kipato sina, mimi ni mzee, watoto wangu ndio wanafanya vibarua huko mjini, kipato ni duni wanachokipata, ndiyo tunanunua maji ya kisima hapo nyumba jirani ndoo ni Sh100,” anasema.

Haji hulazimika kununua ndoo tisa za maji ya kisima na moja ya majisafi kwa Sh500 kila siku ili kukidhi mahitaji. Hii ina maana atalipa wastani wa Sh1,400 kununua ndoo tisa za maji ya kisima na moja ya majisafi ya Dawasa wakati mkazi aliyeunganishwa atatumia Sh1,663 kupata lita 1,000.

Mkazi wa Mbagala, Jamila Musa (36), aliliambia Mwananchi kuwa hutumia Sh1,400 kila siku kununua maji ya kisima kwa ajili ya matumizi ya nyumbani ikiwemo kufua, kupikia na kusafisha nyumba na Sh500 kununua ndoo moja ya yale ya Dawasa kwa ajili ya kunywa na kupikia chai.

“Familia yangu bajeti yangu ya maji kwa siku ni ndoo 14 ambazo ni Sh1,400 na dumu moja la maji ya kunywa. Nina familia ya watoto sita ambao wanatumia maji kuoga na matumizi mengine ya nyumbani, huku kwetu tunanunua ya visima ambayo yana chumvi nyingi huwezi kumudu kupikia chai au kunywa,” anasema Jamila, fundi cherehani ambaye hutumia Sh60,000 kwa huduma hiyo kwa mwezi.

Mkazi wa Goba, Hellen Lyimo anasema: “Nimeishi Kijitonyama kwa miaka mingi na huko nilikuwa nyumba ya kupanga, maji niliyapata bila tatizo lolote, lakini nilipohamia huku maji yamekuwa mtihani, kila siku watoto wanaugua UTI kutokana na maji chumvi ambayo hata hivyo hupatikana kwa nadra na bei ghali.”

Mkazi mwingine wa Goba Oysterbay, Daudi James anasema hulazimika kununua uniti tano za maji ya Dawasa kila mwezi kwa Sh60,000 kwa ajili ya familia yake ya watu sita.

“Ndugu yangu maji ni big issue (suala kubwa) huku. Nanunua uniti moja ya maji ya Dawasa kwa Sh13,000 na nikitaka ya chumvi ni Sh10,000 kwa uniti wakati tungekuwa tumeungwa kwenye mfumo wa Dawasa ningelipa Sh1, 663 kwa uniti,” anasema James.

Hali ni tofauti kwa Gilbert Ndimbo, mkazi wa Mbezi Beach ambaye anasema familia yake hutumia kati ya Sh10,000 na Sh20,000 kulipia huduma ya maji ya Dawasa kwa mwezi mmoja.

“Familia yangu haina sababu ya kununua maji hata dukani, tunapata majisafi kutoka Dawasa na tunamudu hata kunywa baada ya kuyachemsha,” anasema.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa jiji wanaofikiwa na maji ya Dawasa waliozungumza na Mwananchi wanasema wanalipa kati ya Sh9,000 hadi Sh40,000 kwa mwezi ili kupata huduma hiyo.

Wadau wa maji

Mkurugenzi Mkazi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Water Aid Tanzania, Ibrahim Kabole anasema mara nyingi watu wanaoishi katika mazingira magumu mijini na vijijini hutumia fedha nyingi kupata huduma ya maji kuliko wanaoishi katika maeneo yaliyopangwa au wenye kipato kikubwa.

Anasema waliwahi kufanya utafiti na kubaini kuwa maeneo mengi ya Dar es Salaam huduma ya maji hupatikana kwa gharama kubwa.

“Tulifanya utafiti wetu hivi karibuni kwa kulinganisha Manispaa ya Temeke katika Kata ya Kibondemaji, tukagundua kwamba wananchi wa kawaida wananunua maji kutoka kwa wanaotembeza kwenye matoroli na dumu moja la maji lita 20 wanalipia Sh500 wakati mwingine mpaka 1,000,” anasema.

Anasema kwa kawaida mtu anayenunua maji Dawasa anauziwa kwa kipimo cha uniti moja kwa Sh1,600.

“Ukitizama dumu la lita 20 ukagawanya lita 1,000 unapata madumu 50 kwa Sh500 ni Sh25,000 unaona huyu mtu ananunua ujazo wa maji uleule kwa Sh25,000 na wa Masaki analipa Sh1,663,” anasema Kabole.

Majibu ya waziri

Akijibu swali hivi karibuni kuwa Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la maji Dar es Salaam, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa alisema tatizo kubwa la maji ni usambazaji na si upatikanaji wake kama watu wengi wanavyoamini.

Alisema kukabiliana na hilo, Serikali itahakikisha kila Mtanzania aliyepo Dar es Salaam atapata maji.

“Si aliye karibu na bomba kuu tu (la maji), lakini hata aliyeko kilomita 20 au 50 toka kwenye bomba kuu,” alisema Profesa Mbarawa.

Mahitaji ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ni lita 542 milioni kwa siku, lakini uzalishaji ni lita 502 hivyo kusababisha upungufu wa lita milioni 42 kwa siku.

“Sasa hivi tuna miradi mingi ambayo tumeianza. Tuna miradi ambayo imegawanyika katika maeneo mawili. Miradi mikubwa ambayo inasimamiwa na Serikali na miradi mingine ambayo inafanywa na Mamlaka ya Maji Dar es Salaam, yaani Dawasa.”

Alisema, “Kwa mfano, tuna mradi mkubwa wa usambazaji maji ambao utakwenda kutatua tatizo la maji Dar es Salaam maeneo kama Goba na maeneo mengine mpaka Bagamoyo. Mradi huo utagharimu takriban Sh105 bilioni. Hivi tunavyozungumza tuko hatua za mwisho za kumpata mkandarasi.”

“Mradi mwingine upo wa kujibu matatizo ya Kisarawe na maeneo ya Pugu. Kama unavyojua maeneo ya kusini mwa Dar es Salaam yana changamoto kubwa ya maji, sasa kuna mradi mwingine ambao unagharimu karibu Sh10.6 bilioni ambao sasa hivi mkandarasi yuko saiti.”

Waziri huyo aliongeza kuwa, “Kuna mradi mwingine unaendelea wa kusambaza maji Salasala na maeneo mbalimbali unagharimu takriban shilingi bilioni 78, hivi tunavyozungumza mkandarasi amefika asilimia zaidi ya 90 ya utekelezaji. Kazi inaenda vizuri na kila kitu kinaenda vizuri.”

Advertisement