VIDEO: Wenye makazi maeneo ya jeshi kaa chonjo

Msemaji wa Jeshi la Wananchi (JWT) Luteni Kanal,Gaudentius Ilonda akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu wavamizi wa maeo ya jeshi nchini.Picha na Said Khamis

Dar es salaam. Kama kuna watu wamejenga maeneo yanayomilikiwa na jeshi, inabidi wakae chonjo.

Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) limetangaza operesheni ya nchi nzima ya kuwaondoa watu wanaoendelea kuwa na makazi katika maeneo ya kambi za jeshi, ikiwa ni siku chache baada ya askari wake kukata mimea ya wananchi mkoani Pwani.

Aprili 25, askari wa JWTZ walibomoa nyumba na kufyeka mimea katika mashamba ya wakazi wa Kijiji cha Tondoroni na Mtaa wa Kisopwa, Mloganzila wilayani Kisarawe kwa maelezo kuwa wamejenga ndani ya eneo la kikosi cha 83 cha jeshi hilo.

Video iliyosambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii inaonyesha mipapai iliyozaa, mimea mingine ikiwa imefyekwa na nyumba kubomolewa huku wananchi wakilalamikia askari kwa kufanya vitendo hivyo na kumuomba Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kuingilia kati.

Lakini video hiyo ndiyo imechagiza jeshi hilo kuanza kampeni hiyo kubwa kwa maelezo kuwa maudhui yamepotoshwa.

“Jeshi limesikitishwa sana na kitendo cha uchonganishi huo wa kusambaza video ili kupotosha umma kuhusu ukweli wa umiliki wa eneo hilo,” alisema Luteni Kanali Gaudentius Ilonda, kaimu mkurugenzi wa habari na uhusiano wa JWTZ, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

“Eneo hilo linamilikiwa kihalali na jeshi na si vinginevyo.”

Kutokana na mazingira hayo, Luteni Kanali Ilonda alisema kuanzia sasa JWTZ itaendesha operesheni ya kuwaondoa wakazi wote waliovamia katika maeneo ya kambi za kijeshi kote nchini.

“Kwa hiyo operesheni hiyo imeshaanza na itaendelea si kwa Kisarawe tu ila katika maeneo ya wavamizi kwenye kambi za jeshi kote nchini,” alisema.

“Tunaomba wananchi wayaachie (kwa kuwa) maeneo hayo si salama kwa maisha yao. Si hekima kulumbana na baadhi ya wananchi. Tunawasihi kuacha mara moja vitendo vya kuvamia maeneo ya jeshi.”

Kumekuwa na mizozo kati ya wananchi na uongozi wa kambi mbalimbali za jeshi na mingine huishia kwa wananchi kupigwa au kuharibiwa mali zao.

Septemba mwaka jana wakati wa maadhimisho ya miaka 54 ya JWTZ, mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, Jenerali Venance Mabeyo alisema maeneo ya kambi yamevamiwa na watu ambao wamejenga makazi na kufungua biashara na kuwataka waanze kuondoka kabla ya hatua kuanza kuchukuliwa.

Baadhi ya wananchi wamekuwa wakidai kuwa waliwahi kufika maeneo hayo kabla ya kambi kuanzishwa, na hivyo walistahili kufidiwa.

Kabla ya kusambaa kwa video hizo, baadhi ya wananchi kutoka Kijiji cha Tondoroni, waliozungumza na Mwananchi walilalamikia uamuzi wa kubomolewa makazi yao wakati kuna kesi waliyofungia mahakamani mwaka 2016, wakihoji uhalali huo kisheria.

Pia, wakazi hao walisema kijiji hicho kilisajiliwa na kutambuliwa rasmi kisheria mwaka 1993 kabla ya Serikali kuanza kupeleka huduma za kijamii, lakini wanasikitishwa na uamuzi wa kuondolewa.

Lakini Luteni Kanali Ilonda alisema hakuna mwananchi anayedai fidia katika maeneo ya wilaya hiyo ya Kisarawe licha ya jeshi kuwavumilia kwa muda mrefu bila kuondoka.

“Tunawapenda sana wananchi wetu. Hili ni jeshi la wananchi, ni jeshi lenye utii kwa sababu linatokana na wananchi ndiyo maana ilitumika diplomasia na wananchi wote walilipwa fidia Sh2.5 bilioni kati ya 2002 na 2006,” alisema.

“Walifungua kesi iliyochelewesha fidia na Serikali ikalipa fidia ya mwisho Sh1.8bilioni mwaka 2012.

“Eneo lenye kesi tunasubiria mpaka uamuzi wa mahakama ukikamilika ndiyo operesheni itafanyika katika kipande hicho cha Tondoroni, lakini usajili wa kijiji ulifutwa mwaka 2004 na walilipwa fidia wote ila baadhi yao waliuza maeneo kwa watu wengine na wengine kuhamia jirani ndani ya kambi.”