Wenye ulemavu wamlilia Mengi, waeleza alivyowasaidia

Muktasari:

  • Baadhi ya watu wenye ulemavu waliowahi kusaidiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi aliyefanriki dunia usiku wa kuamikia Mei 2, 2019 wameangua kilio baada ya kufika msibani kwa mfanyabiashara huyo leo Jumapili Mei 5, 2019

Dar es Salaam. Baadhi ya watu wenye ulemavu waliowahi kusaidiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi aliyefanriki dunia usiku wa kuamikia Mei 2, 2019 wameangua kilio baada ya kufika katika msiba wa mfanyabiashara huyo leo Jumapili Mei 5, 2019.

Walemavu hao walishindwa kujizuia baada ya kufika katika geti la nyumba ya Mengi, Kinondoni jijini Dar es Salaam na kueleza jinsi wanavyomkumbuka mfanyabiashara huyo.

Jackson Madale, mkazi wa Tiptop amesema amemfahamu Mengi zaidi ya miaka 20 iliyopita alipokwenda ofisini kwake  kumuomba msaada.

Amesema amemsaidia mambo mengi ikiwamo kumsomeshea mwanaye alikuwa amefaulu kuingia kidato cha kwanza, lakini kutokana na kukosa ada Mengi alimlipia mwaka mzima.

"Mengi amenisaidia sana sitasahau mwanangu alipofaulu kijiunga na kidato cha kwanza nilikuwa sina hata 100 nlipokwenda kwake nilimkuta msaidizi wake anaitwa Joyce, akaniambia nikamchukulie fomu za shule," amesema Madale.

Naye Sikujua Mbwembwe amesema Mengi ni mtu aliyekuwa anajali watu wasiojiweza.

“Nakumbuka nilikwenda kwake nikiwa na shida ninalia, Mengi aliniambia niseme neno moja tu ‘I can’ baada ya mwezi mmoja nilitwaa tuzo ya sanaa,” amesema Mbwewe na kuongeza:

"Inafika mahali Mengi anatuita njoo tule chakula cha mchana pamoja, huu ni upendo wa kutosha." 

Mbwewe amesema wamefurahia  mambo mengi sana kwa kipindi chote walichokuwa na Mengi.

Mwingine ni Mohamed Issa ambaye amesema: Mengi ni baba yetu ametufanyia mengi ametupa nguvu na ujasiri.”

Amesema aliwaambia wasiwe watu wa kukata tamaa akawa anarudiarudia neno hilo kila siku.

“Kila aliyekuwa anakwenda kumuona Mengi alikuwa anafanikiwa na hata wale waliokuwa hawana namna yakupata riziki akiwawekea utaratibu.

"Sijui tutafanyaje kuondoka kwa Mengi, alitutia moyo tusiwe watu wakukata tamaa na neno hili akirirudia mara kwa mara na wengi tumefanikiwa.

Naye Rukia Khamis amesema alikuta na Mengi mwaka 1993 akiwa Chuo cha Ufundi cha Yombo alipokwenda kuzindua ujenzi wa sekondari ya watu  wazima iliyobuniwa na walimu wakishirikiana na wananchi wakati akisomea ukarani muhtasi.

"Katika hafla hiyo kulikuwa na nyimbo, ngonjera na maigizo ambayo nilishiriki kikamilifu sanjari na kusoma risala kwa mgeni ramsi (Mengi) ambaye aliahidi kusaidia ujenzi wa sekondari na alifanya hivyo. Baada ya kumalizika kwa shughuli Mengi aliniambia niende ofisi kwake kesho yake," amesema Rukia.

Rukia amesimulia kuwa baada ya kwenda ofisini kwa mfanyabiashara huyo, aliuliza kozi aliyokuwa anasomea katika shule hiyo huku akimpongeza kwa ujasiri aliounyesha wakati wa hafla hiyo.

"Aliniuliza nimesoma sekondari, nikamwambia hapana. Akaniuliza je, ungependa kusoma nikamjibu ndiyo. Baada ya maelezo hayo Mengi aliniahidi kunilipia ada ya mwaka mzima sanjari kunipa Sh5,000 ya matumizi kila mwezi," amesema Rukia.

Amesema taarifa za kifo chake, zimemhuzunisha sana na kwamba kwa hatua aliyofikia ikiwamo kufanya kazi katika maeneo mbalimbali imechangiwa na mfanyabiashara huyo.

"Sasa hivi najivunia fani yangu ya usekretari lakini isingekuwa Mengi nisingefika namshukuru sana kwa moyo wake wa kujitolea kusaidia watu wa kada mbalimbali bila kujali kabila, dini wala rangi," amesema Rukia akionekana mtu mwenye huzuni.

Naye Sylvester Joseph aliungana na Rukia kwa kusema enzi za uhai wake, Mengi alikuwa ni hodari na mpenda maendeleo anayependa kusikiliza matatizo ya wananchi.

"Nilikutana na Mengi mwaka 2008 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili nilikokuwa nikipatiwa matibabu baada ya kupata ajali wilayani Tarime. Mengi alifika kuangalia wagonjwa lakini sikusita kumweleza shida yangu akaahidi kunisaidia.

"Alinisaidia kwenye matibabu hadi leo hii nimepata ahueni licha ya kupata ulemavu namshukuru sana kwa moyo wake. Mengi ni mtu mwenye moyo tofauti aliyejishusha.

"Ukibahatika kukutana na Mengi na kumweleza shida zako hasiti kukusaidia kutokana na utu na upendo aliokuwa nao wakati wote," amesema Joseph.