WhatsApp si salama, fanya haya uwe salama

Wednesday May 15 2019

WhatsApp , salama, fanya , uwe ,salama,wadukuzi,hackers, AFP,

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kama unapendelea kutuma taarifa muhimu na nyeti kwa kutumia mtandao wa WhatsApp, kutuma picha au video, sasa unapaswa kuuhuisha (update) katika simu yako ya mkononi baada ya wadukuzi kufanikiwa kujipenyeza.

Kutokana na kile kilichokuwa kikielezwa kuwa haikuwa rahisi kwa mtu kudukua mawasiliano ya WhatsApp, wengi wamekuwa wakivutiwa na mtandao huo na kuutumia kutuma taarifa muhimu na mazungumzo ya faragha.

Lakini jana, wamiliki wa mtandao huo wametahadharisha kuwa kuna hatari ya kudukuliwa kutokana na kuwepo na taarifa za maharamia wa kimtandao (hackers) waliovamia mtandao huo ambao una watumiaji zaidi ya bilioni 1.5 ulimwenguni kote.

“WhatsApp inahamasisha watu kuhuisha toleo la mwisho la programu katika simu zao sanjari na kuhuisha mfumo wa simu zao ili kuepuka mpango wa udukuzi uliopangwa dhidi yao, lakini pia kulinda taarifa zao binafsi,” imeeleza taarifa iliyonukuliwa na AFP.

Hata hivyo, WhatsApp hawajabainisha idadi ya watu walioathirika na udukuzi huo, lakini virusi hivyo vinaweza kuingia katika simu aina ya Android, iPhone na vifaa vyote vinavyotumia WhatsApp.

Taarifa za mwanzo za kuwepo kwa hofu ya kudukuliwa kwa mtandao huo ziliripotiwa na tovuti ya Financial Times ambayo ilieleza kuwa mbinu inayotumika ni mlengwa kupigiwa simu au kutumiwa ujumbe ambapo utaambatana na virusi ambavyo vitasaidia udukuzi huo.

Financial Times ilisema virusi hivyo vimetengenezwa na kampuni ya Kiisraeli ijulikanayo kama NSO Group ambayo imekuwa ikituhumiwa kwa kushirikiana na Serikali mbalimbali kukabiliana na wanaharakati na waandishi wa habari.

Pia wachunguzi wa usalama wamesema virusi hivyo vinaonekana kufanana na teknolojia mbalimbali zilizowahi kutengenezwa na NSO, hiyo ni kwa mujibu wa mtandao wa New York Times.

Hata hivyo, jana taarifa ya NSO ambayo imewahi kutuhumiwa kushiriki tukio la udukuaji wa taarifa za mwanaharakati wa Umoja wa Falme za Kiarabu mwaka 2016, imeeleza kuwa leseni yake ni kutengeneza mifumo ya kuisaidia Serikali kupambana na uhalifu.

“Tunachunguza madai yote ya kuaminika ya matumizi mabaya ya mtandao. Kama kuna haja tunachukua hatua ikiwa ni pamoja na kuzima mfumo husika,” inaeleza taarifa ya kampuni hiyo bila kukubali wala kukataa kuhusikia na udukuzi wa WhatsApp.

Advertisement