Wiki ya simanzi vifo vitano nchini

Dar/mikoani. Hii ni wiki ya majonzi. Tanzania imepoteza watu watano maarufu kwa nyakati tofauti ndani ya siku nne.

Waliofariki dunia ni aliyekuwa naibu waziri kiongozi wa Zanzibar, Ali Juma Shamuhuna, waziri wa zamani wa Tamisemi, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi, aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Ali Fereji Tamim, mfanyabiashara maarufu wa madini, Thomas Mollel na mwanahabari wa siku nyingi, Nechi Lyimo.

Ngwilizi alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi katika Hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam, wakati Shamuhuna alifariki Jumapili huko Fuoni Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ambako alikuwa akiugua na siku hiyo hiyo Tamim alifariki katika Hospitali ya Mnazi Mmoja. Mollel ambaye alikuwa maarufu kwa jina la Askofu alifariki dunia juzi usiku jijini Dodoma na Lyimo alipoteza maisha jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.

Kifo cha Ngwilizi

Wakazi wa Lushoto na baadhi ya wabunge wa wilaya hiyo walimwelezea Brigedia Jenerali Ngwilizi kama kiongozi wa mfano huku wakisema kifo chake kimewashtua kwa sababu hawakufahamu kama mbunge huyo kuanzia mwaka 2005 na 2015, alikuwa akigua.

Zahabu Mjata wa Kijiji cha Moa, Mlalo alisema Brigedia Ngwilizi amewaachia simanzi kwa sababu licha ya kustaafu ubunge aliendelea kuwasaidia wananchi walipokuwa na shida mbalimbali.

Mkazi wa Kijiji cha Fyevyei, Mlalo, Jamal Hamis alimwelezea Brigedia Ngwilizi ambaye kati ya mwaka 1993 hadi 2004, alishika nafasi mbalimbali za utumishi serikalini ikiwamo Mkurugenzi wa Jiji na baadaye mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwamba alikuwa kiongozi asiyependa ubabaishaji na alitaka ukweli wakati akitatua migogoro ya wananchi waliomfuata.

Mbunge wa zamani wa Bumbuli, William Shelukindo alisema kifo cha Ngwilizi kimempa mshtuko kwa sababu alikuwa mwenzake na kiongozi mwadilifu kwa Taifa.

Mbunge wa sasa wa Mlalo, Rashid Shangazi alisema atamkumbuka Ngwilizi ambaye aliongoza vikosi vya jeshi la ulinzi kuzima uasi katika Visiwa vya Shelisheli na kuiongoza nchi hiyo hadi alipokabidhi kwa Serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, kama mzazi na mtangulizi wake aliyekuwa akimuongoza katika maendeleo ya Jimbo la Mlalo.

Askofu Mollel na Nechi Lyimo

Akizungumzia kifo cha Mollel, katibu mwenezi wa CCM Wilaya ya Meru, Joshua Hungura alisema mfanyabiashara huyo alikwenda Dodoma kushuhudia kuapishwa kwa mbunge wa Arumeru Mashariki (CCM), Dk John Pallangyo.

Alisema juzi saa nne usiku walikula chakula cha jioni pamoja na hakuwa na tatizo lolote.

Mollel, ambaye mwaka 1995 alipata umaarufu baada ya kugawa fedha akiwa ghorofani mjini Arusha huku wananchi wakiziokota chini, alifariki dunia saa tano usiku muda mfupi baada ya kutoka kuoga akiwa na mkewe, “alifariki ghafla akiwa ametoka kuoga baada ya kudondoka mlangoni.”

Hungura alisema Mollel ambaye pia alikuwa mjumbe wa kamati ya siasa ya CCM Wilaya ya Meru na mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM ya wilaya hiyo, siku za nyuma alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa sukari na shinikizo la damu.

Enzi za uhai wake, Mollel alikuwa pia mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite na aliwahi kumiliki timu ya mpira wa miguu ya Pallsons iliyowahi kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara. Pia, amewahi kuwa diwani wa Mbughuni.

Lyimo, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Kilimanjaro (Meck), aliwahi kuwa mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Redio 0ne na Redio Sauti ya Injili, Kilimanjaro.

Katibu wa Meck, Nakajumo James alisema klabu hiyo imepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwandishi huyo mkongwe mkoani Kilimanjaro.

“Nechi Lyimo nitamkumbuka kwa mambo Mengi, ila mawili ni lile aliloripoti katika kipindi cha Mambo Mseto kuhusu Moshi mji wa wagumu na ile ya sanamu ya Askari katika eneo la YMCA kuhusu watu wa Uru,” alisema Rehema Abrahamu.

Shamuhuna na Tamim

Kifo cha Shamuhuna ambaye alizikwa juzi huko Donge Eneani, Kaskazini Unguja aliwahi pia kuwa waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aliongoza mamia ya wananchi katika mazishi hayo.

Marehemu Shamuhuna aliwahi kuwa katibu mkuu Wizara ya Kilimo mwaka 1988 hadi 1990 na aliwahi kuwa mjumbe wa kuteuliwa wa Baraza la Wawakilishi (BLW) mwaka 1995 hadi 2000 ambako pia aliwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitia (BLW).

Aliwahi pia Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Waziri wa Ardhi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango.

Tamim aliyeiongoza ZFA kwa zaidi ya miaka 20, alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu na mwaka jana alifanyiwa upasuaji huko India.

Katika uongozi wake ZFA, alishiriki kikamilifu katika jitihada za kuiombea Zanzibar uanachama wa Fifa.

Imeandikwa na Burhani Yakub, Florah Temba na Haji Mtumwa.