Wilaya kumi zinazoongoza kwa malaria zatengewa Sh12.5 bilioni

Tuesday October 23 2018

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali inatarajia kutumia Sh12.5 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa programu mbalimbali zitakazosaidia kupunguza ugonjwa wa malaria katika wilaya 10 zilizoonyesha kuwa na kiwango cha juu cha maambukizi.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliwaambia wadau waliohudhuria uzinduzi wa pili wa Matokeo ya Utafiti wa Viashiria vya Malaria Tanzania (TMIS) 2017, kuwa fedha hizo zitatumika kwa ununuzi wa viuatilifu vya kuua mazalia ya mbu na vifaa tiba vya kupimia ugonjwa huo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa matokeo hayo jana, Ummy alisema baada ya maambukizi ya malaria kupungua na kufikia asilimia 7.3 kwa mwaka 2017 kutoka asilimia 14.4 mwaka 2015, Serikali itajikita katika kuharibu mazalia ya mbu.

“Tumefikiria kuzielekeza katika maeneo yenye shida ya maambukizi na wilaya zenye kiwango kikubwa cha malaria, kwa sasa ni Kakonko kwa asilimia 30.8, Kasulu 27.6, Kibondo 25.8, Uvinza 25.4, Kigoma 25.1, Buhigwe 24, Geita 22.4, Nanyamba 19.5, Muleba 19.4 na Mtwara 19.1,” alisema Ummy.

Alisema Serikali itajikita kuimarisha upimaji kabla ya kupata dawa na kuhakikisha idadi kubwa ya watu wanatumia vyandarua vilivyowekwa dawa.

“Tuna Sh3 bilioni ambazo tutazielekeza kwenye ununuzi wa viuatilifu kwa ajili ya wilaya zenye maambukizi ya juu, pia tulibajeti kununua dawa nyingi za malaria kwa mwaka 2018. Tuna Dola za Marekani 4.2 milioni (zaidi ya Sh10 bilioni), kwa hiyo hatukununua dawa, tumekaa na wenzetu wa Global Fund wiki jana na tumekubaliana kwamba hizi fedha tunanunua vitendanishi.”

Alisema sasa Serikali itatumia fedha nyingi kununua vipimo vya malaria badala ya dawa. “Ninataka kuwashauri Watanzania tusitumie dawa bila kupima, tunakuja na mpango wa kutaka hata vipimo vya malaria viwekwe katika maduka ya dawa badala mtu aende kwenye kipimo cha afya anajipima mwenyewe,” alisema Waziri Ummy.

Alisema Serikali inahitaji kuwekeza zaidi kwenye kuangamiza mazalia ya mbu na kuweka huduma za kupima karibu zaidi pamoja na matumizi ya vyandarua. Ummy alizitaja halmashauri zenye maambukizi ya chini ya asilimia moja kuwa ni Mbulu TC, Mbulu DC, Hanang, Hai, Siha, Moshi MC, Mwanga, Kondoa TC, Meru DC, Arusha CC, Monduli, Ngorongoro na Rombo DC.

Alisema lengo la Serikali ni kufikia kiwango cha chini ya asilimia moja ifikapo mwaka 2020 na kutokomeza kabisa malaria mwaka 2030. “Katika hili ninawaagiza wakuu wa wilaya, waganga wakuu wilaya, mabwana na mabibi afya pamoja na maofisa afya wote kuhakikisha mnaanza mara moja kushughulika na utokomezaji wa malaria kwa kuangalia namna ya kuondoa mazalia ya mbu, nitamwomba Waziri Tamisemi, (Selemani) Jafo asaini (mkataba wa makubaliano) nanyi tutawapima kuona mmefanikisha vipi,” alisema.

Mtakwimu mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa akitoa utafiti huo, alisema uzinduzi wa kwanza ulionyesha kiwango cha maambukizi kimepungua kwa karibu nusu yaani asilimia 7.3 kutoka asilimia 14.4 mwaka 2015.

Alisema takwimu za maambukizi ya malaria katika ngazi ya halmashauri ni kwa mara ya kwanza zimefanyika tangu NBS ianze kufanya tafiti hizo kuanzia mwaka 2000.

“Ukiangalia takwimu za hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2017 ambao umeendelea kukua kwa asilimia 7.1 ukilinganisha na asilimia 7.0 mwaka 2016, tafsiri ya haraka ni kwamba baadhi ya shughuli za kiuchumi kama vile za afya na huduma za jamii zimechangia kwenye ukuaji huo,” alisema Dk Chuwa.

Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Salma Kikwete alisema sasa ni wakati muafaka kwa halmashauri zenye viwango vya juu vya maambukizi kuangalia uwezekano wa kununua viuatilifu katika kiwanda cha Kibaha ili kutokomeza malaria katika maeneo yao.


Advertisement