Wimbi la wanachama CUF kutimka lamtisha Lipumba

Mwenyekiti wa CUF, Ibrahim Lipumba akikumbatiana na Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (kushoto) aliyekuwa akimuunga mkono Maalim Seif baada ya kutangaza kurejea jijini Dar es Salam jana. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Katibu mkuu mpya wa CUF, Suleiman Khalifa Suleiman alisema kubadilisha ofisi na kupeperusha bendera za ACT-Wazalendo katika majengo yaliyokuwa yakitumiwa na CUF ni kinyume cha utaratibu kwa kuwa ofisi hizo zilijengwa kwa nguvu ya wanachama na siyo mtu.

Dar es Salaam. Wimbi la wanachama wa CUF wanaomuunga mkono aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, limemtisha mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba.

Kufuatia hali hiyo, Profesa Lipumba amewaangukia wanachama wa chama hicho kutoondoka, badala yake wabaki ili wajenge chama na kutibu majeraha yaliyotokana na mgogoro wa kiuongozi uliodumu kwa miaka mitatu.

“Msifuate Maalim Seif, bakini tuijenge CUF, tumetoka mbali hasa wanachama wa Pemba. Maalim Seif ni mharibifu na ameangukia ACT-Wazalendo ambayo ipo mahututi,” alitoa wito huo jana wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi kuu ya makao makuu ya chama hicho Buguruni, Dar es Salaam.

Maalim Seif tayari ametimkia ACT-Wazalendo ambako amekabidhiwa kadi namba moja ya uanachama pamoja na wafuasi wake wakiwamo waliokuwa viongozi wa juu wa CUF upande wa Zanzibar.

Profesa Lipumba aliwataka wanachama wa CUF hasa Zanzibar kuacha kufuata mkumbo kwenda chama kingine akiisema Maalim Seif alikidhoofisha chama hicho na kusababisha mgogoro na ndio maana wamemfuta uanachama.

“Wananchi, wanachama wa CUF hasa Zanzibar hiki ni chama kimoja, endeleeni kukiunga mkono na tutibu majeraha. Tumetoka mbali katika kudai haki nchi hii, CUF ndiyo ilikuwa mstari wa mbele kudai haki ya kupata Katiba mpya, Tume huru ya uchaguzi na utawala bora,” alisema.

Profesa Lipumba alisema, “hiki ni chama cha watu siyo mtu mmoja, msikubali kushawishiwa na mtu yeyote kwenda chama kingine na kuacha uwekezaji mlioanzisha wa kudai haki sawa kwa wote. Wazanzibar mmejitahidi kwa kipindi kirefu kupigania haki zetu, Seif Sharif asitugombanishe.”

Mbali na hilo, Profesa Lipumba alisema licha ya kumfukuza uanachama Maalim Seif, mkutano mkuu uliomalizika Machi 15 uliazimia pia kuwafukuza viongozi wengine ambao ni Ismail Jussa, Salim Bimani, Issa Kheri, Mohammed Nuru na Said Ali Mbarouk wote kutoka Zanzibar pamoja na Joran Bashange, Mbarara Maharagande na Abdallah Katawi wa Tanzania Bara kwa madai ya kushabikia na kuongeza kesi za CUF.

Katibu mkuu mpya wa CUF, Suleiman Khalifa Suleiman alisema kubadilisha ofisi na kupeperusha bendera za ACT-Wazalendo katika majengo yaliyokuwa yakitumiwa na CUF ni kinyume cha utaratibu kwa kuwa ofisi hizo zilijengwa kwa nguvu ya wanachama na siyo mtu.

Khalifa ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Gando - Pemba, alisema kinachofanywa na watu wanaodaiwa kumuunga mkono Maalim Seif si sahihi, lakini wao watatumia utaratibu wa kisheria kuzirejesha ofisi hizo.

“Hatutatumia nguvu katika suala hili, bali tutafuata utaratibu wa kisheria kwa sababu kinachofanyika ni uhuni. Seif anataka kuiba ofisi hizi, lakini hatafanikiwa,” alisema Khalifa.

Katika hatua nyingine, Hamidu Bobali, mbunge wa Mchinga jana alitangaza kurejea kumuunga mkono Profesa Lipumba. Awali, mbunge huyo alikuwa upande wa Maalim Seif. “Nawaomba mnisamehe kwa yaliyotokea nimerudi kukijenga chama chetu,” alisema Bobali.