Wizara tatu kushirikiana kuandaa timu za taifa za riadha na ndondi

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamis Kigwangallah akimaliza mbio za kilomita 21 za Ngoromgoro akitumia muda wa madaa 2:48

Muktasari:

  • Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangallah amesema ili timu za taifa  za riadha na ngumi ziweze kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ni muhimu kuunganisha nguvu ya wizara tatu ili kuandaa timu hizo na kuwalipa vizuri wachezaji kutoka katika majeshi na katika klabu zao.

Karatu. Wizara tatu zinatarajiwa kuungana kuandaa timu ya taifa ya riadha na ndondi ili kuhakikisha Tanzania inafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa na kutangaza utalii.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangallah alitoa kauli hiyo jana mjini Karatu mara baada ya kumalizika mashindano ya riadha ya Ngorongoro ambayo kwa mara nyingine tena washindi  wa kwanza kilomita 21 wametoka nchi jirani ya Kenya.

Waziri Kigwangallah atamuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili kuzikutanisha wizara tatu, wizara ya maliasili na utalii, wizara ya ulinzi na wizara ya mambo ya ndani ili kuunganisha nguvu kupata timu bora za taifa za michezo hiyo.

"Michezo ina nafasi kubwa kulitangaza taifa na kuvutia watalii zaidi hivyo, kama wizara tatu tukishirikiana kuandaa timu bora za taifa kwa kutoa vijana katika majeshi na klabu Tanzania itafanya vizuri sana," alisema.

Alisema kwa kuanzia wizara yake kupitia mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro itaanza mwaka huu ujenzi wa kituo cha kisasa cha michezo ambacho kitaandaa vijana katika mashindano ya riadha ya kimataifa.

"Tuna fursa nzuri kama taifa kufanya vizuri zaidi katika michezo, tumeanza katika soka timu yetu ya Taifa itashiriki mashindano ya mataifa ya Afrika nchini Misri Mwaka huu na tunataka mafanikio haya yaende pia kwenye riadha na Ngumi," alisema.

Mwenyekiti wa bodi ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, Profesa Abuhudi Kaswamila alisema mamlaka hiyo itaendelea kusaidia sekta ya michezo nchin ili kutangaza vivutio vya utalii na kuelimisha vita dhidi ya ujangili.

Katibu Mkuu wa TOC,  Philbet Bay akisoma risala kuhusiana na mashindano ya riadha ya Ngorongoro alipongeza jitihada za wizara ya maliasili na utalii na mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya katika kukuza riadha nchini.

"Kuna mafanikio makubwa yanaonekana kuanzia kwenye mbio hizi za Ngorongoro na tuna imani kituo cha michezo kitakachojengwa kitasaidia sana sekta ya michezo nchini," alisema.