Wizara ya Afya yatoa tahadhari uwapo wa dengue Tanzania

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma leo kuhusu kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya Dengue nchini. Jumla ya watu 307 wamebainikwa kuwa na ugonjwa huo kati ya hao 252 kutoka mkoani Dar es Salaam na 55 kutoka Tanga. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amekiri kuwapo kwa wagonjwa waliobainika na homa ya dengue huku akiviagiza vituo vya afya kote kuhakikisha vinawapima wagonjwa virusi vya ugonjwa huo pindi watakapowabaini hawana malaria

Dar es Salaam. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto imekiri kuwapo kwa ugonjwa wa homa ya dengue nchini, huku Dar es Salaam ikiwa na wagonjwa zaidi ya 200 waliobainika.

Akizungumza na Mwananchi mapema wiki hii, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amesema mikoa ya Dar es Salaam na Tanga imebainika kuwapo kwa wagonjwa wa homa hiyo.

“Tatizo la homa ya dengue tunalo, kwa sasa tumeanza kubaini wagonjwa waliougua Dar es Salaam na Tanga hatujapata vifo vyovyote mpaka sasa tunao wagonjwa takriban 200 Dar es Salaam lakini hakuna aliyeathirika, nashauri watoa huduma kuwapima wagonjwa iwapo watabainika wanaumwa wapewe tiba stahiki,” amesema Dk Ndugulile na kuongeza:

“Asilimia zaidi ya 70 ya homa tulizonazo si malaria, kuna UTI, homa ya matumbo haya yote yanasababishwa na virusi na dengue ni moja ya inayosababishwa na virusi, hatuwezi kukataa kwamba haupo upo ndani ya Tanzania tunachokifanya sasa ni kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na kuwa na takwimu sahihi kwenye hospitali za umma na binafsi.”

Hata hivyo, Dk Ndugulile amewataka wananchi wa maeneo tajwa kuchukua tahadhari ikiwamo kufukia maji na kujikinga na mbu.