Wizara ya Kilimo kujenga maabara kuu

Monday June 10 2019

Mkemia mkuu idara ya chakula ya usalama wa

Mkemia mkuu idara ya chakula ya usalama wa chakula nchini Clepin Josephat akizungumza na wadau wa kilimo ambao wanajihusisha na usalama wa chakula nchini, juu ya mradi wa kudhibiti Sumukuvu katika mazao ya chakula nchini(TANIPAC),wakiwa mkoani Morogoro. 

By Lilian Lucas, Mwananchi [email protected]

Morogoro.  Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kupitia mradi wa kudhibiti sumukuvu katika mazao ya chakula nchini (Tanipac) katika kukabiliana na changamoto ya usalama wa chakula imelenga kujenga maabara kuu ya kilimo yenye uwezo ya kutoa majibu yatakayokubalika kimataifa.

Mkemia mkuu wa idara ya usalama wa chakula nchini, Clepin Josephat amesema hayo leo Jumatatu ya Juni 10, 2019, wakati akizungumza na wadau wa kilimo ambao wanajihusisha na usalama wa chakula nchini.

Josephat alisema mradi huo utakuwa na vipengele vitatu na moja ya vipengele hivyo ni kutokuwa na miundombinu ya kutosha katika kudhibiti masuala ya ubora wa chakula na ujenzi wa maabara hiyo utakaogharimu kiasi cha shilingi20 bilioni huku uimarishwaji wa kituo cha utafiti wa magonjwa ya kibaiolojia kilichopo Kibaha ukifanyika pia.

Mkemia huyo ambaye pia ni mratibu wa utekelezaji mradi wa sumukuvu nchini, alisema pia kutajengwa kituo cha  usimamizi mazao baada ya kuvunwa  katika katika kituo cha mazao cha Kibaigwa na kwamba kujengwa kwa vituo na maabara hizo ni kutokana na uchunguzi uliofanywa na watafiti wa kilimo baada ya kuwepo kwa uchafuzi wa kemikali ya sumukuvu katika mazao ya chakula hususani mahindi na karanga.

“Baada ya kutokea kwa athari hizo katika mazao ya chakula iliandaliwa andiko na kukubalika na baadaye kupata fedha ambazo zitakabiliana na tatizo hilo, nia yetu ni kuongeza mauzo ya nje na ni lazima tuhakikishe kwa udhibiti wa mazao uende katika utaratibu unaotakiwa,”alisema Josephat.

Alisema wadau wa kilimo watapatiwa mafunzo kwa ajili ya udhibiti katika mikoa 10 itakayofikiwa, huku wakulima 6,000 kutoka halmashauri 18 nchini watafikiwa kwani kama wataalamu wamegundua kuwa masuala mengi ya Sumukuvu hayaeleweki kwa watu wengi kuanzia kwa watu wa kawaida na wale wa juu wenye maamuzi.

Pia alisema kwa kuwa mwananchi ndio mzalishaji wa mazao hayo lazima wafikiwe kwa wakati na haraka kwani wakati wa uchunguzi chanzo kikuu cha sumukuvu hiyo ilikuwa ni mvua ambazo zilinyesha bila kutegemewa na mazao kunyeshewa yakiwa bado shambani hivyo baada ya kuvunwa hayakutunzwa vyema na kusababisha sumukuvu kuota.

Meneja mradi wa Tanipac kwa upande wa Zanzibar Mwanaidi Ally Khatibu alisema kuwa kwa upande wake kutajengwa maghala mawili kwa ajili ya uhifadhi wa mazao ya nafaka na katika eneo jingine katika mnyororo wa tathamani taasisi zinazojihusisha na chakula kama ZFDA zitawezeshwa katika masuala ya kilimo.

Khatibu alisema tatizo lililopo watu wengi hawaelewi sumukuvu hivyo watatoa elimu juu ya nadhara yake na kwa bahati mbaya kwa Zanziba ukubwa wa tatizo halijajulikana.

Kaimu ofisa wa Kilimo,Umwagiliaji na Ushirika Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Ntirankiza Misibo amesema sumukuvu imekuwa tatizo katika eneo lake hasa katika mazao ya alizeti, mahindi na karanga hivyo kama itadhibitiwa kuna uwezekano mkubwa wa wakulima kuondokana na athari hivyo.

Advertisement