Wizara ya mambo ya ndani kumwaga ajira lukuki

Wednesday April 24 2019

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi 

By Habel Chidawali,Mwananchi [email protected]

Dodoma. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetenga ajira 5,400 katika mwaka wa fedha 2019/20, huku nyingi zikielekewa kwa jeshi la polisi.

Waziri wa wizara hiyo, Kangi Lugola amesema hayo leo Jumatano Aprili 24 bungeni mjini Dodoma  wakati akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/20 bungeni jijini Dodoma.

Waziri Lugola amesema bado kuna uhaba wa rasilimali watu hivyo wizara hiyo imetenga ajira hizo kupunguza uhaba huo.

Katika mgawanyo huo, polisi wataajiri askari 3,725, magereza 685, huku zimamoto na uhamiaji kila mmoja akipewa nafasi za ajira 500 kwa kipindi hicho.

Kwa kauli hiyo, huenda agizo la Rais John Magufuli alilotoa wakati akizundua mji wa kiserikali jijini Dodoma hivi karibuni kuhusu vijana wa kujitolea waliojenga majengo ya Serikali wapatiwe ajira limeanza kutekelezwa.

Rais aliagiza vijana hao 1,500 kuajiriwa wote katika vikosi vya ulinzi na usalama, ambapo alimtaka mkuu wa majeshi kushirikiana na idara nyingine ili wagawane kuwapa ajira vijana hao wa JKT.

Advertisement