Ney wa Mitego: Woga umewakimbiza wasanii kwenye miondoko ya Hip Hop

Muktasari:

Miongoni mwa wasanii waliokomaa na miondoko ya muziki wa Hip Hop ni Emmanuel Elibariki maarufu Ney wa Mitego. Akifanya mahojiano maalumu na Mwananchi pamoja na mambo mengine alizungumzia wasanii kuikimbia miondoko ya Hip Hop na kukimbilia kwenye muziki wa biashara.

Miongoni mwa wasanii waliokomaa na miondoko ya muziki wa Hip Hop ni Emmanuel Elibariki maarufu Ney wa Mitego. Akifanya mahojiano maalumu na Mwananchi pamoja na mambo mengine alizungumzia wasanii kuikimbia miondoko ya Hip Hop na kukimbilia kwenye muziki wa biashara.

Swali: Kinachoonekana ni kama muziki wa miondoko ya Hip Hop umefifia, tatizo nini?

Ney: Miondoko hiyo haiwezi kufifia, wala kufa, ila wasanii ndiyo wanaikimbia. Pamoja na sababu za kibiashara kwa kuwa miondoko hiyo haijawahi kuwa na soko hapa nchini, wameangalia nini kinalipa na wamekwenda kufanya kila mmoja anatafuta riziki, pia wasanii ni waoga wanafanya vitu laini.

Hata mimi ndiyo maana sitabiriki ninafanya muziki wote, narap , naimba lengo ni kuhakikisha gemu la muziki linabaki na vitu vikali.

Swali: Waoga kivipi?

Ney: Maana ya Hip Hop ni kutetea, kufanya harakati za ukombozi siyo kusifia na kuremba. Utamu wa miondoko hiyo kuongeza vitu vyenye uhalisia, uoga wa wasanii unakuja hapo.

Wakati uliopo siyo rafiki, sijui niseme viongozi, Serikali hawataki kusikia ukizungumza ukweli na uwazi ukifanya hivyo utaonekana wimbo wako una ukakasi.

Ambao tulijaribu kukomaa kama mimi na Roma Mkatoliki yaliyotukuta hakuna asiyejua, hivyo msanii kuingia huko anaona atajipoteza au kupoteza muda kujibu tuhuma.

Hivyo kuliko kuimba miondoko hiyo kwa mashairi laini ambayo hayaendani na uhalisia wake wameona bora watokomee kabisa.

Swali: Mashabiki wanapenda Hip Hop?

Ney: Ukiimba vitu vya maana wanapenda , lakini ukiimba vitu laini laini wanasema hiyo siyo Hip Hop.

Hata hivyo hapa nchini muziki huo hauna mashabiki wengi, tofauti na Marekani ambapo wasanii wanaouimba ni matajiri.

Huku imekuwa tofauti kabisa, nahisi Watanzania wanapenda zaidi kusikiliza kuhusu mapenzi ndiyo maana Bongofleva imewashika.

Swali: Miondoko ya Bongofleva na Hip Hop ipi nyimbo zake zinadumu?

Ney: Hip Hop inaishi kwa sababu ni maisha halisi ya watu, sauti ya wasiokuwa nayo, mtetezi wa wanyonge, Bongofleva kila siku inabadilika na ni muziki wa biashara itafikia wakati watu watachoka watataka kusikia vitu vya maana.

Hapo Hip Hop itarudi na wasanii walioikimbia miondoko hiyo lakini wanaiweza watarudi pia kufanya kazi.

Swali: Wimbo gani kati ya nyimbo zako unaamini hukufanya kazi ya bure?

Ney: Karbu zote nilitulia, lakini “Alisema”, niliumiza kichwa mashairi yake yapo poa, nilizungumza vitu vya msingi, ikiwamo vile ambavyo watu hawavizungumzi.

Bila shaka sikupoteza wimbo huo hadi sasa unaishi na utaishi muda mrefu.