Ya Rugemalira, Seth ni yaleyale mahakamani

Watuhumiwa wa kesi ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi, James Rugemalira na Harbinder Sethi wakitoka katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo, baada ya kesi inayowakabili kuahirishwa hadi julai 4, 2019 kutokana na upelelezi kutokamilika. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Upelelezi katika kesi ya uhujumu uchumi, Habinder Seth na James Rugamalila umekwamisha kuendelea kwa kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam nchini Tanzania


Dar es Salaam. Washtakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi, Habinder Seth na James Rugamalira wanaendelea kusota rumande takribani miaka miwili, kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokukamilika.

Washtakiwa hao wanaokabiliwa na mashtaka 12.

Wakili wa Takukuru, Leonard Swai amedai leo Juni 20, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Huruma Shaidi kuwa shauri limekuja kwa ajili ya kutajwa na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine kutokana na upelelezi kutokamilika.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 4,2019 itakapotajwa tena na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Katika shtaka la kwanza washtakiwa wanadaiwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19,2014 jijini Dar es Salaam, walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India kwa ajili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika shitàka la pili la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao kati ya Oktoba 18,2011 na Machi 19,2014 jijini Dar es Salaam wakiwa sio watumishi wa umma walitekeleza mtandao huo wa uharibifu kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shtaka la tatu, Sethi anadaiwa Oktoba 10, 2011, katika mtaa wa Ohio Ilala Dar es Salaam, akiwa ana nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 ya usajili ya kampuni na kuonyesha yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua ni uongo.