Zaha aipeleka Ivory Coast robo fainali

Muktasari:

  • Licha ya kuzidiwa na wapinzani wao Mali, Ivory Coast imefuzu robo fainali ya Kombe la Mataifa Afrika kwa ushindi wa bao 1-0 jana usiku.

Cairo, Misri. Bao la mshambuliaji nyota wa Crystal Palace Wilfried Zaha limeipeleka Ivory Coast robo fainali ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon).

Zaha alifunga bao hilo dakika ya 76 kwa kiki ya karibu na kuipa ushindi wa bao 1-0 Ivory Coast dhidi Mali jana usiku.

Nyota huyo anayehusishwa na mpango wa kutua Arsenal katika usajili wa majira ya kiangazi, alifunga bao hilo akiwa karibu na kipa wa Mali Djigui Diarra.

Mali iliyotawala mchezo, ilikosa nafasi za kufunga kupitia kwa wachezaji Moussa Marega na Moussa Djenepo ambao walishindwa kuweka mpira wavuni licha ya kuwa eneo zuri.

Ivory Coast iliyotwaa ubingwa wa Afrika mwaka 1992 na 2015, haikuwa katika kiwango bora kulinganisha na Mali iliyocheza soka ya kuvutia.

Timu hiyo yenye idadi kubwa ya nyota wanaocheza ligi maarufu Ulaya ilicheza chini ya kiwango hasa kipindi cha kwanza cha mchezo huO.

Djenepo, anayetarajiwa kujiunga na Southampton majira ya kiangazi, alikosa nafasi ya kuikomboa Mali licha ya kupata nafasi nzuri kadhaa za kufunga.

Pia kiki ya Abdoulay Diaby ilipanguliwa na kipa wa Ivory Coast kabla ya Djenepo kupoteza nafasi nyingine ya kufunga.

Katika mchezo mwingine, Tunisia ilifuzu robo fainali kwa ushindi wa mabao 5-4 iliyopata dhidi ya Ghana kwa penalti, baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 120.