Zaidi ya mikoa minane kufungwa mashine 62 za uchujaji damu

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa msaada wa mashine 62 za kusafisha figo zenye thamani ya shilingi 1.5 bilioni kutoka kwa Naibu balozi wa Saudi Arabia nchini, Ahmed bin Saleh Alghamdi (kulia) jijini Dar es Salaam leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Wagonjwa wa figo waliotembea umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma ya kusafishwa damu, wamepunguziwa safari baada ya Serikali kuelekeza mashine 62 zilizotolewa na Ubalozi wa Saudi Arabia kufungwa katika hospitali za rufaa za mikoa zaidi ya nane bara na visiwani

Dar es Salaam. Serikali imesema inapeleka mashine za kuchuja damu kwa wagonjwa wa figo, zitakazofungwa katika hospitali za rufaa za mikoa zaidi ya mikoa nane bara na visiwani yenye uhitaji ili kuwapunguzia safari wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.

Akizungumza na vyombo vya habari Leo Juni 17, 2019 wakati akipokea msaada wa mashine hizo 62 zenye thamani ya Sh1.550 bilioni kutoka Ubalozi wa Saudi Arabia, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile amesema mashine hizo zitaelekezwa mikoani ili kupunguza changamoto kwa wagonjwa hao.

“Mgonjwa wa figo anayehitaji kusafishwa damu lazima akae katika mashine Mara tatu mpaka nne kila wiki kwa maisha yake yote mpaka atakapopandikizwa figo nyingine ni changamoto kwa walio wengi kwanza ilikuwa umbali wa huduma na gharama za usafidhaji ambapo mpaka sasa ni Sh250,000 kwa awamu moja hivyo mgonjwa kuhitaji Sh1 milioni kila wiki,” amesema.

Dk Ndugulile amesema kupatikana kwa mashine hizo kunaifanya nchi kuwa na mashine 275 nchi nzima, hivyo huduma ikisogezwa mikoani itabaki changamoto ya gharama kwa wagonjwa.

Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni pamoja na Tanga, Kigoma, Bukoba, Arusha, Iringa, Mwanza, Mtwara, Unguja na Pemba