Ziara ya JPM Ruvuma na Njombe ilivyoacha matumaini mengi

Hivi karibuni Rais John Magufuli alihitimisha ziara ya kikazi katika mikoa ya Kusni na Nyanda za Juu Kusini ambako alishiriki shughuli balimbali hasa za kimaendeleo.

Ziara hiyo ilimfikisha Rais Magufuli mkoani Mtwara, Ruvuma, Njombe na Iringa ambako alipata fursa ya kukutana na viongozi na kuwahutubia wananchi ambapo katika baadhi ya hotuba alitoa msimamo wa Serikali juu ya mambo mbalimbali.

Kati ya mambo aliyoyafanya ni pamoja na kuzindua, kuweka mawe ya msingi na kukagua miradi 9 yenye thamani ya Sh519 bilioni mkoani Ruvuma.

Akizindua kiwanda cha kuchakata majani ya chai mabichi cha Kabambe, kilichopo Njombe mjini, Rais Magufuli alisema ni vyema mawaziri wa fedha na viwanda na biashara wakashirikiana na wabunge kuangalia namna watakavyowasaidia wananchi na wawekezaji.

Rais Magufuli alikubaliana na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cook aliyesema kuwa kuna changamoto katika uwekezaji, hali inayosabababisha wanaotaka kuwekeza kuachana na mpango huo.

“Mtu akitaka kuwekeza anapata shida na masharti ya ajabu ajabu. Nakubaliana na (balozi) Cook kuwa baadhi ya watendaji wa Serikali ni tatizo katika masuala ya uwekezaji,” alisema Rais Magufuli.

“Wanamuona mwekezaji kama adui, badala ya rafiki. Watendaji wabadilike, mtu anataka kuwekeza kiwanda lakini anazungushwa mwaka mzima, watu wetu wamekuwa na vichwa vigumu nafuu ya kamongo ‘samaki jamii ya kambale’ hawataki kuelewa.”

Rais alifafanua kuwa kuna baadhi ya wawekezaji waliofika nchini lakini waliwekewa mikwara na kuamua kutimkia nchi za jirani, huku wengine wakiombwa rushwa ili mipango yao ya kuwekeza ifanikiwe.

Fedha za wahisani

Akiwa Madaba mkoani humo, Rais Magufuli alitaja sababu za kupeleka fedha za wahisani moja kwa moja kwenye miradi ya wananchi kuwa inatokana na kutumiwa vibaya na baadhi ya watendaji.

Rais alisema alipokuwa akizindua Kituo cha Afya Madaba kuwa, baada ya fedha za wadau kutumiwa vibaya kila zinapotolewa waliamua ziwe zinapelekwa moja kwa moja kwenye miradi husika.

“Lazima tuseme kweli. Siyo kwamba wafadhili wetu walikuwa hawatoi fedha za afya, siku za nyuma walikuwa wakitoa lakini watendaji wetu katika halmashauri walikuwa wakizitafuna, lakini sasa tumeamua fedha hizo zinakwenda moja kwa moja kwenye zahanati au kituo cha afya,” alisema.

Katika uzinduzi huo Sh650 milioni zilitumika kwenye ujenzi wa kituo hicho, kati ya fedha hizo Sh220 milioni zilinunua vifaa.

Akiwa katika ziara hiyo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema uboreshaji wa miundombinu katika vituo vya kutolea huduma za afya umeongeza idadi ya akina mama kujifungua katika vituo vya afya.

Alisema kabla ya uboreshaji huo akina mama hasa wa mkoa wa Ruvuma waliokuwa wanajifungua katika vituo vya afya walikuwa chini ya asilimia 63.

Miundombinu, maji

Aprili 6, mwaka huu akiwa katika ziara hiyo wilayani Tunduru, alimtaka Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa kukaa na wataalamu wa zizara yake kwani wamekuwa wakifanya vibaya na miradi mingi ya maji haikamiliki na ipo mingine ni ‘hewa’.

“Nilikupeleka Wizara ya Maji ukafanye mabadiliko, lakini bado unashindwa kuwachukulia hatua wahandisi wa maji ambao hawasimamii kikamilifu miradi ya maji,” alisema Rais Magufuli wakati akizungumza na wananchi wa Tunduru mkoani Ruvuma.

Katika ziara hiyo pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli alizindua barabara ya Namtumbo-Kilimasera, Matemanga-Tunduru yenye urefu wa kilomita 193 iliyogharimu Sh148.9 bilioni. “Haifurahishi kuona wananchi wanalalamikia ukosefu wa maji, ni uzembe. Wafukuze wakandarasi wa maji na chukua hatua kwa mainjinia wa maji ambao wanafanya vibaya, ukiwa mpole miradi haitakamilika.”

“Tunafikiria kuchimba maji mita 20 ilhali yanapita mita zero kule juu, hapa kuna mpaka wa Tanzania na Msumbiji ambao ni Mto Ruvuma usiokauka.”

Rais Magufuli alimuagiza Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa kushughulikia mradi wa maji wa Manga uliopo Makambako mkoani Njombe.

Kutokana na malalamiko ya wananchi mkoani humo na baadaye kupata maelezo kutoka kwa viongozi wa mji wa Makambako kuwa mradi huo ulijengwa ukiwa na mabomba yasiyohimili maji yanayopita eneo hilo, Rais Magufuli alimuagiza Waziri Mbarawa kubaki mjini Makambako ili ashughulikie tatizo hilo.

Rais Magufuli alisema suala la maji Makambako linaonekana kuwa tatizo.Alisema katika Sh117 bilioni za miradi ya maji, fedha halali ni Sh17 bilioni huku nyingine zote zikichapwa (zimeliwa).