Zitto: Maalim Seif ndio turufu yetu Zanzibar - VIDEO

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akizungumza alipokuwa akihojiwa na waandishi wa Mwananchi Communications Limited, jijini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amemzungumzia aliyekuwa katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye hivi karibuni alijiungana chama hicho akisema nguli huyo wa siasa nchini Tanzania ni turufu ya chama hicho kufanya vizuri viziwani Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe amesema Maalim Seif Sharif Hamad ndio turufu ya chama hicho kuzoa ushindi katika majimbo ya Zanzibar kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Zitto ametoa kauli hiyo jana Jumanne Juni 4, 2019 katika mahojiano na Mwananchi baada ya kuulizwa nafasi ya ACT-Wazalendo visiwani Zanzibar baada ya Maalim Seif kujiunga na chama hicho akitokea CUF.

“Kwa upande wa Zanzibar sisi (ACT-Wazalendo) ni Serikali tunayosubiri maana mpaka sasa tuna uwezo wa kushinda majimbo ya ubunge yasiyopungua 28 na uwakilishi yasiyopungua 28 kati ya majimbo 50 ya Zanzibar.”

“Tuna rekodi ya ushindi wa upinzani Zanzibar  tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi. ACT-Wazalendo ni chama kipya Zanzibar na hakina makandokando. Zanzibar hatuna mashaka sisi ni Serikali inayosubiri,” amesema Zitto.

Akieleza jinsi Maalim Seif alivyoshawishika kujiunga na ACT-Wazalendo, Zitto amesema, “Sisi hatukuwa Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) lakini ndio chama kilichotoa msimamo mkali baada ya matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar kufutwa. Jambo hilo lilikonga nyoyo za Wazanzibari na walituona tunalia nao licha ya kuwa hatukuwepo katika Ukawa.”

“ACT-Wazalendo tulitangaza wazi kutomtambua Dk Shein ( Ali Mohamed-Rais wa Zanzibar) kama rais halali tuliona kaingia kwa mapinduzi si uchaguzi halali. Uchaguzi halali ulifanyika Oktoba 2015 na aliyechaguliwa alipaswa kutangazwa ambaye ni Maalim Seif.”

Amesema hayo waliyafanya kwa dhamira ya dhati bila kujua kuwa kuna siku Maalim Seif atajiunga na chama hicho.

“Sasa wakati tunasema hayo walituona na ilipofikia mahali wanataka jukwaa la kufanya siasa walielezwa hawakuwa na sisi katika Ukawa lakini tulilia nao wakaungana nasi.”

Ukawa ulijumuisha vyama vya NCCR-Mageuzi, NLD, Chadema na CUF wakati huo kabla ya Maalim Seif kukihama.

“Hili ni funzo kubwa kwa maana ya kutenda wema na kwenda zako Mungu atakuja kulipa tu. Tuna furaha kwa sababu tumekuwa chama kikubwa na tumepata uzoefu wa kutosha kutoka kwa Maalim na wenzake,” amesema Zitto.

Amesema Maalim Seif ni kiongozi anayeweza kufananishwa na Nelson Mandela (Rais wa kwanza Mwafrika wa Afrika Kusini), Raila Odinga (Kiongozi wa Upinzani nchini Kenya) kutokana na jitihada na harakati zake.

“Amekuwa kila siku katika mapambano na hajateteleka, anaanguka lakini hakati tamaa anaendelea. Amesimamia msimamo wa kuhakikisha Wazanzibari na Watanzania  wanapata haki yao ya kidemokrasia. Anapaswa kupata nishani, kuheshimiwa ni bahati mbaya hatukumpa heshima anayostahili,” amesema Zitto.