Zitto aeleza mikakati ya ACT-Wazalendo Dar

Saturday July 13 2019

 

By Tausi Ally, Mwananchi [email protected] co.tz

Dar es Salaam. Viongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo nchini Tanzania wametakiwa kutatua changamoto zilizopo katika mitaa yao.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Julai 13, 2019 na kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe katika mkutano wa wajumbe 83 wa majimbo 10 ya mkoa huo.

Majimbo hayo ni Ubungo, Mbagala, Kinondoni, Ilala, Segerea, Ukonga, kibamba, Kigamboni, Temeke na Kawe.

"Lengo la mkutano ni kujadiliana, kujitazama na kujitathmini kutokana na majukumu mbalimbali katika uimarishaji wa chama  Mkoa wa Dar es Salaam na kuangalia wapi tunafanya vizuri na wapi tunafanya vibaya,” amesema Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini.

Amesema katika mkutano huo wanapanga ajenda ya kuzungumza katika kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba 13, 2019.

Amesema  wanataka kuwa na ilani ya uchaguzi ya Mkoa wa Dar es Salaam itakayobainisha mitaa iliyopo na changamoto sambamba na jinsi ya kuzitatua.

Advertisement

"Mitaa Dar es Salaam ipo zaidi ya 561 tuna kazi kuhakikisha tunapata watu wenye uzoefu ambao wataondoa changamoto hizo ikiwemo ya mafuriko,” amesema Zitto.

Kuhusu takataka, mbunge huyo wa Kigoma mjini  amesema Dar es Salaam inatengeneza taka nyingi zinazoziba mifumo ya kupitisha maji taka huku miundombinu hiyo ikiwa haiendani na ongezeko la watu.

“Kama chama lazima tuwe na majibu katika hili, ndio maana tumekutana hapa,” amesema Zitto.

Katibu wa Chama hicho, Catherine Semhando amesema katika uchaguzi huo wamejipanga kuhakikisha wanachukua viti vingi vya wenyeviti wa serikali za mitaa na kuigeuza Dar es Salaam kuwa ya zambarau, rangi ya bendera ya chama hicho.

 

 


Advertisement