Zitto ahoji mambo matatu bungeni

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe akichangia bungeni mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe amehoji mambo matatu bungeni ambayo ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kutumia sheria ipi kukubaliana na washtakiwa kulipa faini au kuwapunguzia adhabu, Takukuru kutokaguliwa pamoja na Wakala wa Ndege za Serikali kuhamishiwa ofisi ya Rais.

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe amehoji mambo matatu bungeni, likiwemo suala la Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DDP) kukubaliana na baadhi ya washtakiwa ambao hulipa ama faini, kupunguziwa adhabu au kufutiwa mashtaka na kuhoji fedha wanazolipa washtakiwa zinakwenda wapi.

Mambo mengine aliyohoji mbunge huyo leo jioni Aprili 12, 2019 wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma na Utawala Bora) ni hesabu za Takukuru kutokaguliwa pamoja na Wakala wa Ndege za Serikali kuhamishiwa ofisi ya Rais.

“Kumekuwa na utamaduni ofisi ya mwendesha mashtaka kukamata watu, hatujui kama wanabambikiwa kesi au la, lakini baadaye tunaona watu wale wanakubaliana na ofisi ya DPP na kulipa pesa na kesi hiyo inakwisha,” amesema Zitto.

“Ningependa nchi yetu ipate ufafanuzi huenda kuna uonevu mkubwa sana, kwamba watu wanabambikiwa kesi kwa utakatishaji fedha wanawekwa ndani ili wazungumze na DPP halafu waende mahakamani wakiri na kulipa faini kiwango ambacho wameshtakiwa nacho.”

Huku akitolea mfano kesi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za Mkononi ya Vodacom Tanzania, Hisham Hendi, aliyekiri mashtaka na kulipa faini,  Zitto amesema;

“Nchi yetu haina sheria wala kanuni zinazowezesha pale ambapo mtu ametuhumiwa kujadiliana na mwendesha mashtaka ili ama kupunguza adhabu, kufuta adhabu au kulipa faini, haya makubaliano ya DPP na watuhumiwa yanaendeshwa kwa sheria ipi?”

Amesema mwaka jana DPP amekusanya zaidi ya Sh23bilioni kwa watu wanaokamatwa  na kumaliza kesi kati yao na DPP, “Tunaomba kufahamu kwa sheria ipi? Fedha zinakwenda wapi na nani anakagua hizo fedha. Hatuwezi kuendesha nchi namna hii naomba tupate maelezo.”

Naibu Waziri wa Viwanda, Stella Manyanya aliomba kutoa taarifa kwa Zitto akimtaka kuwasilisha mambo anayoyazungumza kwa maandishi ili iwe rahisi kufuatilia.

Zitto hakujibu taarifa hiyo na kuendelea,”Takukuru ndio taasisi ambayo tumeipa dhamana ya kupambana na rushwa, bajeti ya mwaka huu tunawaombea Sh75bilioni, ila taarifa nilizonazo miaka minane iliyopita Takukuru hesabu zake hazijawahi kukaguliwa na mkaguzi yeyote yule.”

“Ni kwanini Takukuru hawakaguliwi wala hawafungi hesabu na kila mwaka wanatengewa mabilioni ya fedha, wanapambana na rushwa lakini hawakaguliwi, Serikali itoe maelezo katika hili.”

Kuhusu wakala wa ndege za Serikali Zitto amesema, “Nimesoma hotuba ya ofisi ya Rais ukurasa wa 87,  Bunge linajulishwa kuwa kwa mujibu wa GN (Gazeti la Serikali) 252 ya 2018 kwa sasa wakala wa ndege za Serikali umehamishiwa ofisi ya Rais kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.”

Ameongeza, “Mwaka 2017/18 tulitenga Sh509bilioni, mwaka unaofuata Sh497bilioni na mwaka huu zinatengwa Sh500bilioni kwa ajili ya ununuzi ya ndege za ATCL (Shirika la Ndege Tanzania), lakini tunajua ATCL hawamiliki ndege wanakodisha zinamilikiwa na wakala wa ndege za Serikali.”

“Halafu tunapitisha huku lakini tunategemea CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) atakagua Wizara ya Ujenzi na tunaambiwa wakala huo upo chini ya ofisi ya rais. Hivi Serikali inataka kuficha nini?”Alihoji Zitto.