VIDEO:Zitto amjibu msajili wa vyama tishio la ACT kufutwa

Muktasari:

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amejibu hoja zilizotolewa na ofisi ya msajili wa vyama vya Siasa kuhusu chama hicho kutumia neno la dini ya Kiislamu la takbir, wanachama wake kutuhumiwa kuchoma moto bendera na kutowasilisha hesabu za chama hicho

Dar es Salaam. Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe amejibu mambo matatu ambayo chama hicho kimeandikiwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa na kutishiwa kufutiwa usajili.

Jana ofisi ya msajili wa vyama vya siasa alikiandikia barua chama hicho na kukipa siku 14 kujieleza kwa nini kisifutiwe usajili kutokana na kufanya mambo matatu ikiwamo kutumia maneno ya dini ya Kiislam ‘takbir’ wakati watu wanaodaiwa kuwa ni wanachama wa ACT Wazalendo walipokuwa wakipandisha bendera ya chama hicho.

Katika barua hiyo iliyosainiwa na naibu msajili wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza ilisema wanachama wa chama hicho  walichoma bendera za CUF jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kutowasilisha taarifa ya hesabu za mwaka wa fedha  2013/14 zilizokaguliwa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG).

Katika mkutano wake na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Zitto amesema madai ya kutowasilisha hesabu za mwaka 2013/14 hayana ukweli.

Amesema wajibu wa chama cha siasa ni kuwasilisha hesabu zake kwa CAG za mwaka 2013/14 ziliwasilishwa kama walivyotakiwa.

Amesema chama hicho kilipata usajili wa kudumu Mei 5, 2014 ikiwa ni miezi miwili kabla ya mwaka wa fedha kuisha Juni 30, 2014.

Ameeleza kuwa kwa kutumia kanuni za kimataifa za hesabu na ushauri wa CAG, waliambiwa wanaweza kuunganisha hesabu za mwaka wa fedha 2013/14 na 2014/15 kwenye ripoti moja ikiunganisha miezi miwili ya taarifa ya mwaka 2013/14.

"Sheria inaruhusu kufanya hivi hata kwa miezi 18 na kabla ya kufanya hivyo tulimwandikia msajili wa vyama vya siasa barua ya January 22 na 29 , 2015 na tukajibiwa barua zote tunazo" amesema Kabwe.

Amesema chama hicho kilikuwa namba moja kupeleka mahesabu yake kwa CAG kukaguliwa na kupata hati safi.

"Msajili angekuwa na nia njema angeweza kuuliza, labda barua zilipotea ofisini kwake tungempa kwa sababu tunazo na sheria ya vyama vya siasa iliyopitishwa hivi karibuni inampa mamlaka ya kuomba nyaraka zozote tungempa," amesema Kabwe.

Kuhusu kuchomwa bendera za CUF, Zitto amesema msajili mwenyewe anaonyesha hana uhakika kama kweli waliofanya hivyo ni wanachama wa ACT Wazalendo.

Amesema chama hicho kina orodha ya wanachama na wanapewa kadi, hivyo wana dhamana na wanachama wao.

Amesema msajili wa vyama vya siasa alipaswa  ajiridhishe anaowatuhumu ni wanachama wa ACT Wazalendo au la.

"Nina uhakika hawezi kwenda mbele ya Mahakama kuthibitisha hilo," amesema.

Kuhusu matumizi ya neno takbir, amesema ni jambo lililowashangaza kwa sababu chama hicho ni cha watu wote ikiwamo wenye dini na wasiokuwa na dini.

Amesema kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho, hawafungamani na dini yoyote ndiyo maana wameruhusiwa kufanya shughuli za siasa.

"Tunafahamu Watanzania wana dini zao, sana maneno yao ya kawaida kutumika hayana maana ya udini, viongozi wote hufungua hutuba zao kwa kusema bwana Yesu asifiwe, tumsifu Yesu Kristo na Assalam aleykum  hatuamini kama kusema hivyo ni udini" amesema.

Amesema jambo hilo wanawaachia wanazuoni walifafanue  kama mwislamu akisema takbir ni udini.

"Sheikh mkuu atoe fatwa kuhusu neno hilo," amesema.

Zitto amedai barua hiyo ya msajili wa vyama vya siasa haina nia njema na waopenda demokrasiaa wote walione kama suala linaloweza kuharibu usalama wa taifa na linaweza kuleta machafuko nchini.

Amesema amani na utulivu  uliopo ni kwa sababu wananchi wana chaguo akichoshwa na CCM atakwena Chadema, Cuf au na kwingineko.