VIDEO: Zitto apinga pendekezo la Serikali kurejesha kodi taulo za kike

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amesema Serikali ya Tanzania imechukua uamuzi wa haraka kutoa pendekezo la kurejesha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)katika taulo za kike mwaka mmoja baada ya kuifuta

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amepinga pendekezo la Serikali ya Tanzania kurejesha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye taulo za kike katika bajeti ijayo ya mwaka 2019/2020 kwa maelezo kuwa ni uamuzi wa haraka na unarudisha nyuma sifa ya Tanzania.

Zitto ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Juni 21, 2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni.

Katika bajeti ya mwaka 2018/19, Serikali iliondoa VAT kwenye taulo za kike lakini bajeti ya 2019/2020 imerejesha kodi hiyo kwa madai ya walengwa kutonufaika.

“Inawezekana Serikali ikawa sawa kwamba bei ya taulo hazijashuka lakini inapaswa kutafakari je mwaka mmoja ambao utekelezaji umefanyika unatosha kupima ilichofanya mwaka jana,” amehoji Zitto.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa ACT- Wazalendo, mwaka jana Serikali ilikuja na pendekezo la kuongeza kodi kwenye mafuta ghafi yanayotoka nje ili kulinda wazalishaji wa mbegu za mafuta nchini lakini jambo hilo halikufanikiwa.

“Mwaka 2017 kabla ya kodi kupandishwa tulikuwa tunazalisha mafuta tani milioni 6.6 lakini  mwaka 2018 tumezalisha tani milioni 1.6, yaani pendekezo ambalo Serikali imelileta mwaka jana matokeo yake hayakuzalisha tegemeo la uzalishaji wa mbegu kuongezeka,” amesema Zitto na kwamba mwaka 2019, Serikali haijaja na pendekezo la kufuta pendekezo hilo.

Kwa kutumia mfano huo, Zitto amesema haiwezekani  pendekezo la kikodi likazaa matunda ndani ya mwaka mmoja.

“Kodi imeanza Julai 2018 kuna watu walikuwa na bidhaa ambazo wamenunua hazikuwa na punguzo hilo lazima watauza kwa bei ile ile, pia fedha yetu imeporomoka thamani dhidi ya dola Ya Marekani na taulo hizi nyingi tunaagiza kutoka nje je tumetazama hili?”

“Serikali itazame vizuri na kutoa muda wa kutosha kama ilivyofanya katika mafuta. Mwaka jana suala la taulo za kike tulikuwa mfano na India, Afrika Kusini na Australia wametuiga,” amesema Zitto.