Zitto ataka mshikamano Zanzibar

Muktasari:

Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema ujasiri na mshikamano ndio njia pekee itakayozaa utawala wa sheria na wenye kuheshimu haki

 

Pemba. Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema ujasiri na mshikamano ndio njia pekee itakayozaa utawala wa sheria na wenye kuheshimu haki.

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Machi 22, 2019  wakati akizungumza na wananchi wa kisiwani Pemba wakiwemo waliokuwa viongozi wa CUF waliojiunga na ACT.

Leo Zitto pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliyejiunga na ACT Machi 18, 2019 wameanza ziara ya siku nne Pemba.

Kiongozi huyo amesema njia pekee ya kuwarejesha Watanzania kwenye utawala unaoheshimu sheria na haki za binadamu ni wananchi walio wengi kushikamana na kuwa kitu kimoja.

“Haki inayotafutwa leo inaweza ikapatika hivyo naomba tushikamane na tusikate tamaa,” amesema Zitto.

Awali, aliyekuwa mratibu wa CUF kisiwani Pemba,  Said Ali Mbarouk alimuhakikishia kiongozi huyo kuwa wananchi wengi wa Pemba wanataka kujiunga na ACT licha ya kutoka mbali na CUF.