VIDEO: Zitto ataka uchaguzi Serikali za mitaa kuwa huru, amtaja Jafo

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akiwa na Mshauri Mkuu wa Chama hicho, Seif Sharif Hamad wakati wakifungua matawi katika kata ya Vingunguti jijini Dar es Salaam leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Chama cha ACT Wazalendo kimezindua matawi 10 katika kata ya Vingunguti ikiwa ni maandalizi ya chama hicho kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo kuhakikisha uchaguzi wa serikali za mitaa unafanyika kwa uhuru na haki.

Zitto ametoa wito huo leo Jumapili Julai 28, 2019  jijini Dar es Salaam wakati akifungua matawi 10 ya chama hicho kata ya Vingunguti, jimbo la Segerea.

Zitto ameambatana na viongozi wengine wa chama hicho akiwemo mshauri wa ACT, Maalim Seif Sharif Hamad na Katibu Mkuu wa chama, Dorothy Semu.

Amesema chama chake kimejiandaa kushinda kwenye uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.

"Natoa wito kwa Waziri wa Tamisemi, Jafo ahakikishe kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa unafanyika kwa uhuru na haki. Tunataka wananchi wakachague viongozi wanaowataka na siyo kuvuruga uchaguzi, hilo hatutakubali," amesema Zitto.

Kwa upande wake, Maalim Seif amewataka vijana kusimama imara katika kutetea demokrasia hapa nchini kwa sababu wao ndiyo nguvu kazi ya Taifa hili na wanaweza kuleta mabadiliko wanayoyataka.

Mwanasiasa huyo mkongwe amewataka vijana kufikiria kesho yao kwa kuleta mabadiliko chanya ambayo yataleta maendeleo katika Taifa hili. Amewataka wawe jasiri kupigania demokrasia na maendeleo ya nchi yao.

"ACT Wazalendo ndiyo chama kinachobeba yale mnayoyahitaji. Malengo yetu ni kuongoza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, matumaini yetu yote ni kwenu vijana," amesema Maalim Seif.

Zitto ameongoza ziara ya wanachama na viongozi wa ACT Wazalendo kuzindua matawi ya chama hicho katika kata ya Vingunguti. Kiongozi huyo ametembea mtaa kwa mtaa na kufungua matawi mapya ya chama hicho.