Zitto ataka wakulima kuwa na mfuko wa hifadhi ya jamii

Muktasari:

  • Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesherehekea sikukuu ya wakulima Nanenane kwa kuwatembelea wafanyabiashara wa soko la Tandale, jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesherehekea sikukuu ya wakulima Nanenane kwa kuwatembelea wafanyabiashara wa soko la Tandale, jijini Dar es Salaam.

Katika ziara yake hiyo Zitto amesisitiza kuanzishwa mfuko wa hifadhi ya jamii kwa ajili ya wakulima.

Amesema mkulima ni muhimu katika kuchangia pato la Taifa na kwamba wana haki ya kuthaminiwa ili kuwatoa katika wimbi la umasikini.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Agosti 8, 2019 wakati akizungumza na wafanyabiashara hao, “ Kuna changamoto katika sekta ya kilimo, ila dawa ni kuanzisha hifadhi ya jamii kwa wakulima. Mfano, katika nchi za wenzetu kuna kitu kinaitwa fao la bei ambapo unaanzishwa mfuko maalumu kwa ajili ya kutunza akiba wakati bei inapokuwa nzuri.”

“Lakini pia bei inapoporomoka mkulima anapewa fidia ya kiwango cha bei. Hii itasaidia kuwainua wakulima nchini ambao wanachangia takribani asilimia 30 ya pato la Taifa lakini tukisema tuendelee kubaki hapa tulipo ambapo bei ikishuka mkulima anaumia hataweza kufukisha uchumi wa taifa mbele.”

Amesema kuanzishwa kwa mfuko huo kutawawezesha wakulima nchini kuwa na akiba zao kupitia vyama vyao vya ushirika ili wasiendelee kuwa alama ya umasikini.

Mfanyabiashara wa matunda, Salimu Shabani amesema biashara ni nzuri licha ya vikwazo mbalimbali na kuiomba Serikali kuanzisha ghala maalumu la kuhifadhia matunda ili yasiharibike.