Zitto awaeleza wapiga kura athari za ACT- Wazalendo kufutwa

Muktasari:

  • Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe aeleza yatakayotokea iwapo chama hicho kitafutiwa usajili na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe ameeleza athari itakayotokea iwapo chama hicho kitafutwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutokana na makosa mbalimbali ikiwamo wanaodaiwa wanachama wa chama hicho kuchoma bendera za CUF.

Amesema Machi 25, 2019 ofisi ya msajili ilikiandikia barua ACT-Wazalendo, ikieleza kusudio la kutaka kukifutia usajili wa kudumu chama hicho kutokana na makosa hayo.

Akizungumza leo Jumatatu Aprili mosi 2019 na wakazi wa Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto amewaambia iwapo chama hicho kikifutwa yeye hatokuwa mbunge wa jimbo hilo na madiwani 19 kati 26 wanaotokana na ACT-Wazalendo watapoteza nafasi hizo.

“Chama kikifutwa mtakosa mwakilishi bungeni, manispaa ya Kigoma Ujiji itavunjika kwa sababu madiwani saba watakaobaki watashindwa kuunda asilimia 50 ya Baraza la Madiwani sanjari na madiwani wengi wa maeneo tofauti.

“Jambo hilo lina maana kuwa sasa watu wa Kigoma Mjini na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla mtakosa mbunge wa kupaza sauti yenu bungeni, mtakosa mbunge wa kwenda kuhimiza kumalizwa kwa mradi wa maji uliocheleweshwa tokea mwaka 2015,” amesema Zitto.

Ameongeza kuwa wakazi wa jimbo hilo watakosa mbunge wa kupaza sauti juu ya uonevu wa watu wa uhamiaji dhidi yao na atakayewapaza sauti kuhusu utaifishwaji wa nyavu za wavuvi Ziwa Tanganyika.

Hata hivyo, Zitto amesema tayari katibu mkuu wa chama hicho, Dorothy Semu leo amewasilisha majibu katika ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa akiwa na ushahidi wa hoja zote zilizotolewa na mlezi huyo wa vyama vya siasa.

Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini amesema zimetimia wiki mbili tangu kumpokea aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliyeambatana na wafuasi mbalimbali.

“Ujio wa Maalim Seif umesababisha matawi zaidi ya 600 ya CUF Zanzibar pamoja na wanachama 125,000 kujiunga na ACT- Wazalendo ndani ya wiki mbili. Sasa hivi chama hiki  kimekuwa kikubwa na tishio mno ndio msingi wa hujuma hizi,” amesema Zitto.