Zoom Tanzania yaruhusu kuuza vitu vilivyotumika mtandaoni

Thursday June 13 2019

By Mwandishi wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kuondokana na tabia ya kuhifadhi vitu visivyotumika, mtandao wa Zoom imeweka kipengele kinachomuwezesha yeyote anayetaka kuuza alichonacho kutafuta wateja.

Tangu ilipoanzishwa na kuanza kutoa huduma zake nchini mwanzoni mwa miaka ya 2000, Zoom Tanzania umekuwa ukiwakutanisha wauzaji wa bidhaa mbalimbali na wanunuzi mtandaoni.

Meneja masoko wa kampuni hiyo, Stephen Swai anasema baada ya mazoea ya mud amrefu sasa wamebadili mfumo ili kupanua wigo na kuruhusu wananchi wengi zaidi kutumia huduma hiyo.

“Mwanzo tulikuwa tunawakutanisha wafanyabiashara na wateja lakini sasa hivi hata wasio wafanyabiashara anaweza kuuza mali walizonazo,” amesema Swai.

Hii ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kuwaruhusu wananchi wa kawaida kuuza wanachotaka baada ya kuona hawawezi kukitumia tena.

“Hakuna kampuni inayoruhusu uuzaji wa vitu vilivyotumika. Wengi wanataka kuuza bidhaa za wafanyabiashara. Wapo watu wanavyo vtu ambavyo hawavitumii, tumewapa nafasi ya kuviuza kabla havijaharibika,’ amesema Swai.

Kwa jukwaa hilo, amesema Watanzania watajiongezea kipato cha ziada kwa kuuza vitu wasivyovihitaji au kuongeza nafasi majumbani mwao kwa kuviondoa vitu hivyo visivyo na tija tena kwao.

Watakaochangamkia fursa hiyo, Swai amesema wataweza kugawana walivyonavyo na wengine wanaovihitaji baada ya wao kumaliza kuvitumia na kutosheka huku wakilipwa kiasi kidogo kulingana na thamani ya mali husika.

“Kila kitu unachodhani hukihitaji, yupo anayekitafuta mahali fulani. Zoom inawakutanisha bila malipo yoyote waweze kutimiza haja zao,’ amesema meneja huyo.

 

 

 


Advertisement