Zuio la viroba lahamia Uganda

Thursday May 16 2019

Waziri wa Biashara na Viwanda wa Uganda, Amelia

Waziri wa Biashara na Viwanda wa Uganda, Amelia Kyambadde 

Kampala, Uganda. Serikali ya Uganda imetangaza  kuanzia Juni mosi 2019 viroba vitakavyokutwa madukani vitateketezwa na watengenezaji watafutiwa leseni.

Waziri wa Biashara na Viwanda wa Uganda, Amelia Kyambadde amenukuliwa na Gazeti la New Vision akisema: “Tumezipa hadi Mei 31 kutekeleza agizo hili wazalishaji wote wa viroba, ikifika Juni mosi leseni zao zinafutwa. Hata kwa vile vinavyoingizwa kutoka nje, wahusika watakumbana na hatua zilezile.”

Amesema wameunda kamati ambayo itakuwa inapita kuhakikisha zuio hilo linatekelezwa, huku akibainisha kuwa hadi sasa kampuni 15 zimetekeleza.

Waziri huyo amesema wameelekeza kampuni husika zibadili vifungashio kutoka viroba kwenda chupa za ujazo kuanzia mililita 200, ambazo zitakuwa zinauzwa si chini ya Sh2,000 za Uganda, ili kupunguza idadi ya wanaomudu pombe hizo.

Kama ilivyokuwa nchini Tanzania, waziri alihusisha viroba hivyo na ongezeko la ajali za pikipiki maarufu bodaboda, akisema kutokana na urahisi wake kubeba wanywaji wanaamua kutumia kilevi  hicho wakiwa kazini.

Mapema mwaka 2017, viroba vilizuiwa nchini Tanzania na katika operesheni zilizofanyika katika viwanda na maghala mbalimbali ya pombe yenye mamilioni ya shilingi zilizofungashwa kwenye viroba hivyo zilikamatwa.

 

Advertisement