Majaliwa atoa maagizo kwa wizara ya kilimo kuboresha zao la mchikichi

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakitazama mbegu ya mchikichi inayoonyesha tabaka la mafuta wakati alipotembelea Kituo cha Utafiti wa Michikichi cha Kihinga mkoani Kigoma leo Jumapili. (Picha na Ofisi ya Waziri )

Muktasari:

  • Leo Jumapili, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametembelea kituo cha utafiti cha zao la michikichi cha Kihinga mkoani Kigoma na kutoa maagizo kwa wizara ya kilimo kuhakikisha zao hilo linazalishwa kwa wingi nchini. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza wizara ya kilimo iwawezeshe watafiti katika kituo cha utafiti cha zao la michikichi cha Kihinga mkoani Kigoma ili waweze kuongeza kasi ya uzalishaji wa mbegu bora za zao hilo.

Amesema Serikali imeamua kuongeza nguvu kwenye zao hilo la michikichi hivyo wizara ya kilimo haina budi kukiwezesha kituo hicho kwa lengo la kuzalisha mbegu bora zitakazosambazwa kwa wakulima.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jumapili, Februari 17, 2019 wakati alipotembelea kituo cha Kihinga kwa ajili ya kukagua shughuli za uzalishaji wa mbegu za michikichi akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma.

Taarifa ya kitengo cha mawasiliano ya ofisi yake imesema, Serikali imeamua kulifufua zao hilo kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini, ambapo kwa mwaka inatumia zaidi ya Sh600 bilioni kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi.

“Wizara ya kilimo iwawezeshe watu wa utafiti ili waendelee na shughuli hiyo kwa kasi, iwaongeze watumishi kituoni hapa na ongezeni nguvu kwenye zao la michikichi kama yalivyofanya mataifa mengine ya Costa Rica na Malaysia,” amesema Majaliwa.

Amesema wakulima wa zao hilo wanahitaji kupata mafanikio, hivyo kituo hakina budi kuongeza nguvu ya uzalishaji wa mbegu bora ili wafikie malengo na pia amewashauri washirikiane na taasisi binafsi zinazozalisha mbegu.

Pia Waziri Mkuu amesema Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Kihinga, kiendelee kutoa elimu na wizara ya kilimo ijenge majengo yake inayoyahitaji kwa ajili ya kufanyia shughuli za utafiti. Eneo la chuo lina ukubwa kwa hekta 920.

Kwa upande wake, Mratibu wa Utafiti wa Kilimo kwa mikoa ya Tabora na Kigoma, Dk Filson Kagimbo amesema michikichi iliyopo sasa ina uwezo wa kuzalisha tani 1.6 ya mawese kwa hekta moja ambao ni uzalishaji mdogo na hauna tija.

Amesema mbegu wanazozizalisha zinalenga kumuongeza tija mkulima kwa kuwa zitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani nne kwa hekta, pia wanaendelea kuangalia vinasaba vya mbegu vilivyopo ili wazalishe mbegu bora zaidi.

Amesema miche ya michikichi inachukua muda wa miezi 18 kutoka hatua ya uchavushaji hadi kusambazwa kwa wakulima.

Baada ya kumaliza shughuli ya ukaguaji wa uzalishaji wa mbegu kituoni hapo, Waziri Mkuu amekagua shamba la michikichi la Gereza la Kwitanga  lenye ukubwa wa ekari 400 na kupanda mche kama ishara ya uzinduzi wa upandaji wa miche bora shambani hapo

Waziri Mkuu amesema Serikali imeamua kuongeza nguvu katika zao hilo na inategemea taasisi zake mbili za Jeshi la Magereza (Kwitanga) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT-Bulombora), ambazo zina mashamba makubwa ya michikichi.

Waziri Mkuu pia ameagiza elimu kuhusu kilimo cha zao la michikichi kuanzia hatua za awali hadi uzalishaji wa mafuta itolewe mashuleni ili wanafunzi waanze kupata uelewa na ifikishwe hadi kwa wananchi.