Serikali ya Tanzania yasema watumishi hawalazimishwi kutumia mtandao wa TTCL

Thursday May 30 2019

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara Habari maelekezo Dk Hassan Abbas akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Siku chache baada ya kusambaa kwa tangazo linalowataka watumishi wote wa Serikali kuwa na laini za mtandao wa simu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas ametoa ufafanuzi kuhusu suala hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Mei 30, 2019 amesema hakuna agizo la Serikali linalolazimisha mfanyakazi serikalini kutumia laini za TTCL wala kupangiwa kutumia mtandao wowote.

Amesema agizo hilo linawahusu viongozi wanaowekewa vocha za Serikali na kutakiwa kuwa na laini hizo ili vocha wanazowekewa ziwe za mtandao huo.

“Tunachotaka ni wale viongozi wanaowekewa vocha watumie mtandao huo, lengo ni kuunga mkono shirika letu na ukweli ni kwamba TTCL iko vizuri hata mimi nimerudi nyumbani kumenoga,” amesema.

Dk Abbas amebainisha kuwa si kweli kuwa waandishi wa habari nao wanatakiwa kuwa na vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo, akitoa ufafanuzi wa kauli iliyotolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi.

Dk Abbas amesema waliolengwa katika tamko hilo la Hapi ni wapiga picha ambao sio waandishi ila wanafanya shughuli hiyo kama wajasiriamali.

Advertisement

“Pale mwandishi anapokuwa na shughuli nje ya uandishi mfano upigaji picha kwenye sherehe au studio ni muhimu kuwa na kitambulisho,” amesema Dk Abbas.

Advertisement