Kitilya wenzake kuendelea kusota mahabusu

Muktasari:

  • Upelelezi wa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Kampuni inayoshughulikia Uwekezaji wa Mitaji na Dhamana (Egma) Harry Kitilya na wenzake wawili haujakamilika.

Dar es Salaam. Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi akiwamo mwenyekiti wa kampuni inayoshughulikia Uwekezaji wa Mitaji na Dhamana (Egma) Harry Kitilya na wenzake wawili wataendelea kusota mahabusu.

Pamoja na Kitilya aliyewahi kuwa kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wengine ni waliokuwa maofisa wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Solomon.

Mshtakiwa Sinare aliwahi kuwa Miss Tanzania mwaka 1996.

Wakili wa Serikali, Patrick Mwita leo Ijumaa Novemba 9, 2018 ameieleza mahakama mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya kutajwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Mwita amedai wanawasiliana na wachunguzi ili wajue upelelezi umefikia wapi.

Baada ya wakili, Mwita kueleza hayo, Hakimu Shaidi ameiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 16, 2018 ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekwisha kamilika ama la.

Washitakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa dola za Marekani milioni 550  kwa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard Uingereza.

Wanadaiwa Machi 2013 jijini Dar es Salaam walijipatia Dola za Marekani milioni sita, wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji upatikanaji wa mkopo  na zililipwa kupitia Kampuni ya Egma T Ltd.

Washitakiwa hao wanadaiwa kutakatisha fedha kwa kuhamisha, kuchukua na kuweka kiasi cha Dola za Marekani milioni sita katika akaunti tofauti tofauti za benki.

Kati ya  Machi 2013 na Septemba 2015, wanadaiwa  kuwa waliweka pesa hizo katika akaunti mbalimbali zilizomilikiwa na kampuni ya Egma na kwamba walipaswa kufahamu kuwa pesa hizo ni mazao ya uhalifu wa kughushi.