Kope, kucha zagawa wabunge Dodoma

Kauli ya Spika kuwapiga marufuku wabunge wanawake wenye kucha na nywele bandia imepokewa kwa hisia tofauti.

 

BY Habel Chidawali, Mwananchi hchidawali@mwananchi.co.tz

IN SUMMARY

  • Wapo wanaounga mkono hoja ya Spika na baadhi wameikosoa kuwa anaingilia uhuru wa watu.

Advertisement

Dodoma. Kauli ya Spika kuwapiga marufuku wabunge wanawake wenye kucha na nywele bandia imepokewa kwa hisia tofauti.

Wapo wanaounga mkono hoja ya Spika na baadhi wameikosoa kuwa anaingilia uhuru wa watu.

Jana katika viunga vya Bunge jijini Dodoma mjadala mkubwa ulikuwa kauli ya kucha na kope bandia. Baadhi ya wabunge walipotoka ndani ya ukumbi wa Bunge kwa mapumziko ya mchana, walikuwa wakitaniana kuhusu masuala hayo.

Juzi, Spika Job Ndugai alipiga marufuku wabunge wanawake kuingia bungeni wakiwa wamebandika kope na kucha bandia.

Ndugai alisema, “Kwa mamlaka niliyopewa na Bunge, napiga marufuku kuanzia leo hakuna mbunge atakayeingia ndani ya Bunge akiwa amebandika kucha au kope za bandia na suala la kujipodoa bado natafuta ushauri na majadiliano na wenzangu.”

Jana, milango ambayo wabunge wanaitumia kuingilia ndani ya jengo hilo haikuwa na ukaguzi mpya tofauti na siku zingine licha ya kuwa askari waliokaa milangoni walikataa kulizungumzia jambo hilo.

Mbunge wa Viti Maalumu, Oliva Semguluka (CCM) aliunga mkono katazo hilo akisema ni aibu kwa mbunge kujibandika kope na kucha bandia na kuingia kukitumikia chombo kikubwa kama Bunge.

Semguluka alisema ni dhambi pia kwa wanawake ambao wameumbwa na Mungu kwa sura na mfano wake. Kufanya hivyo, alisema ni sawa na kuukosoa uumbaji wa Mungu na ni ulimbukeni.

Mbunge wa Hanang’, Dk Mary Nagu (CCM) alisema urembo kwa wanawake ni mzuri, lakini unatakiwa kutozidi kipimo.

Ester Bulaya (Bunda Mjini-Chadema) alisema kauli ya spika inapaswa kupingwa na wabunge wanawake kwa sababu huo ni udhalilishaji.

Alisema kila mmoja ana uhuru wake wa namna ya kujipamba, akifanya hivyo, atakuwa anaingilia uhuru wao.

Alihoji kwa nini, Spika hakuzungumzia madhara ya uvutaji wa sigara kwa wabunge wanaume.

Alisema wapo wabunge wanaume wanaotumia vilevi na wakati mwingine huingia bungeni wakiwa na pombe kichwani, lakini hajawapiga marufuku.

Lakini Zainab Vullu (Viti Maalumu-CCM) alisema kauli ya Spika liwe funzo kwa wanawake wote, si wabunge pekee.

Alisema kila mwanamke akitambua madhara yatokanayo na vipodozi, atawajibika sasa kutunza asili ya ngozi na viungo vyake alivyozaliwa navyo badala ya kuvibandikia vya bandia.

Alihoji kwa nini hali hii inaendekezwa na wanawake Wakiafrika tu, mbona Wazungu hawafanyi hivyo?

Mbunge mwingine aliyepinga amri ya Spika ni Rhoda Kunchela (Viti Maalumu-Chadema) aliyesema kabla ya kutoa amri hiyo, naibu waziri wa afya alishasema kucha na kope hazina madhara, bali inategemea na matumizi yake hivyo hakukuwa na sababu ya kupiga marufuku.

Wabunge wanaume wazungumza

Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM), aliunga mkono kauli ya Spika na akaenda mbele zaidi kutaka nywele bandia nazo zipigwe marufuku.

Keisy alisema urembo wa wanawake unaliumiza Taifa kwa sababu fedha nyingi zinatumika kununua vitu vingi ambavyo havina tija na vina madhara.

Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Vedasto Ngombale (CUF) alisema kujiremba kwa wabunge au wanawake wa Kitanzania siyo jambo baya, ila usipite kiwango.

Ngombale alisema kujiremba anakozungumzia Ndugai ni kule kulikopitiliza ambako mwisho wa siku husababisha vilio kwa watumiaji wenyewe na jamii inayowazunguka.

More From Mwananchi
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept