Korti yakataa kupokea bangi kesi ya Wema Sepetu

Muktasari:

  • Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kusikiliza hoja zilizowasilishwa na Wakili wa Serikali, Costantine Kakula na wakili wa utetezi, Tundu Lissu.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekataa kupokea msokoto na vipisi viwili vya bangi vilivyotolewa na upande wa mashtaka kama sehemu ya ushahidi katika kesi inayomkabili Wema Sepetu na wenzake wawili.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kusikiliza hoja zilizowasilishwa na Wakili wa Serikali, Costantine Kakula na wakili wa utetezi, Tundu Lissu.

Awali, akiongozwa na Kakula kutoa ushahidi, akiwa shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, Elias Mulima kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali alidai alipima msokoto na vipisi viwili vinavyodaiwa kukutwa nyumbani kwa Wema na kugundua kuwa ni bangi.

Mulima kupitia kwa wakili Kakula aliiomba Mahakama kupokea bahasha iliyokuwa imefungwa yenye namba ya maabara 291/2017 ikiwa na muhuri na saini yake kama kielelezo cha ushahidi wake kuhusu bangi hiyo. Baada ya bahasha kupokewa na Mahakama, Kakula alimuuliza shahidi iwapo anakumbuka kuna vitu gani ndani ya bahasha hiyo?

Mulima alidai ndani ya bahasha hiyo kuna msokoto mmoja na vipisi viwili ambavyo ndani vina majani ya bangi.

Kakula alimtaka shahidi aifungue bahasha hiyo. Baada ya kuifungua alitoa vitu hivyo na kuiomba Mahakama kuvipokea kama kielelezo, ombi lililopingwa na wakili Lissu akidai ndani ya bahasha hiyo kuna vitu zaidi ya msokoto mmoja na vipisi viwili vinavyodaiwa kuwa ni bangi.

Alidai kuwa kwa kuviangalia kwa makini vitu hivyo, ni vipisi vya sigara ya kienyeji ambayo imetumika kwa kuwa vina alama ya kuungua ambayo kwao vinaitwa twagooso.

Lissu alibainisha kuwa, kitu kinachoitwa msokoto wa bangi hakijulikani kwa kuwa kimefungwafungwa tu kwenye karatasi.

Alidai haiwezekani vitu vilivyotolewa kwenye bahasha kuwa ndivyo shahidi alivyovielezea, hivyo kuiomba Mahakama isikubali kuvipokea kama kielelezo.

Wakili Kakula alidai kuwa pingamizi za upande wa utetezi hazina msingi kisheria kwa kuwa wakati shahidi anatoa ushahidi, alieleza vitu vilivyokuwamo ndani ya bahasha kuwa ni msokoto mmoja na vipisi viwili vya bangi. Aliiomba Mahakama kuvipokea kama kielelezo.

Lissu alisisitiza kuwa, kila kilichomo kwenye bahasha hiyo iliyofungwa kilipaswa kutajwa kwa kuwa wateja wake wanakabiliwa na shtaka ambalo wakibainika wana hatia watafungwa.

Hakimu Simba alitoa uamuzi wa kukataa kupokea vitu hiyo kama kielelezo na aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 12 na 13 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka.

Wema na wenzake Angelina Msigwa na Matrida Abbas wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na dawa za kulevya na kutumia dawa hizo.

Inadaiwa kuwa Februari 4, katika makazi ya Wema yaliyoko Kunduchi Ununio, washtakiwa walikamatwa wakiwa na msokoto mmoja na vipisi viwili vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.

Wema pia anadaiwa kuwa Februari Mosi katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam, alitumia bangi.

Watatu kumtetea Masogange

Katika kesi nyingine inayomkabili msanii, Agnes Gerald maarufu Masogange mahakamani hapo, mashahidi watatu watamtetea.

Jana, Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri alitoa uamuzi wa kumuona Masogange ana kesi ya kujibu ya kutumia dawa za kulevya hivyo kusema anapaswa kujitetea baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake.

Baada ya uamuzi huo, mshtakiwa huyo alieleza kuwa atajitetea kwa njia ya kiapo na anatarajia kuwaita mashahidi watatu. Anatetewa na mawakili Nehemia Nkoko na Ruben Simwanza.

Upande wa mashtaka unaowakilishwa na Wakili wa Serikali, Kakula uliwaita mashahidi watatu.

Masogange (28) anayekabiliwa na mashtaka mawili ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin na oxazepam ataanza kujitetea Oktoba 12.