Kucha, kope bandia za wabunge zazua mjadala mkubwa mtandaoni

Siku moja baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuzuia wabunge wanawake kuingia bungeni wakiwa wamebandika kope na kucha bandia, zuio hilo limezua mjadala mitandaoni.

 

BY Asna Kaniki, Mwananchi akaniki@mwananchi.co.tz

IN SUMMARY

  • Zawaibua wanaharakati,  wanamitindo na wanasiasa.

Advertisement

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuzuia wabunge wanawake kuingia bungeni wakiwa wamebandika kope na kucha bandia, zuio hilo limezua mjadala mitandaoni.

Spika alitangaza zuio hilo jana bungeni muda mfupi baada ya Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndungulile kutoa majibu ya madhara yanayowapata wanawake wanaotumia kucha na kope za bandia.

Wananchi hao wametoa maoni yao kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, ambapo baadhi wameunga mkono na wengine kupinga.

Mwanamitindo, Flaviani Matata ameandika hivi kwenye ukurasa wake: “Nimesoma sehemu kuwa wabunge wanawake hawaruhusiwi kubandika kucha wala kope, kwa hiyo watakuwa wakikaguliwa?, tuna matatizo na changamoto nyingi kama nchi ‘for us to be worried with personal issue like this’ (za kushughulikia badala ya kuhangaika na masuala ya mtu kama haya).”

Naye Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema ameandika:

“Mamlaka ya Spika yanapaswa kuwa na nguvu na uwezo kwa kusimamia Serikali katika mambo ya msingi, Mheshimiwa Tundu Lisu (Mbunge) hajawahi kuwa na hadhi ya ubunge toka aliposhambuliwa kwa risasi lakini leo tumeona mamlaka ya Spika yakiweza kuwa imara katika vita ya kucha na kope za wanawake wabunge.”

Kwa upande wake, mwanaharakati Maria Sarungi ameandika katika ukurasa wake akisema:

“Hivi kwa sasa concern kubwa ya bunge ni makucha ya kubandika? Ndo tatizo mkianza kukubali kupangiwa vitu mwisho unaingiliwa uhuru wako binafsi. Acha wabunge wajitetee maana hata sheria kandamizi walio wengi wanasema ndiyoo.”

Naye Mwanahaisi Singano katika ukurasa wake alitoa maoni kuwa: “Tuliwapeleka kwa kura nyiingi bungeni ili wakatutetee kwa hiyo wanatakiwa kwa hilo wajitetee wenyewe.”

Akizungumza bungeni jana, Waziri Ndungulile alisema takribani wagonjwa 700 hupokewa kwa mwaka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwa na matatizo yatokanayo na kumeza vidonge vinavyobadili sura pamoja na vipodozi vyenye kemikali na kwamba watu hao wapo kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya ngozi.

Soma zaidi: Wabunge wanawake wenye kucha, kope za kubandika wapigwa ‘stop’ bungeni

More From Mwananchi
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept