Lema: Millya alihama siku nyingi Chadema

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.

Muktasari:

  • Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amezungumzia uamuzi wa James Millya kuamua kujiuzulu ubunge na kuhamia CCM akisema matendo na mienendo yake ilionyesha toka awali kuwa amehama Chadema

Dar es Salaam. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema aliyekuwa mbunge wa Simanjiro, James Millya alihama siku nyingi ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Oktoba 7, 2018 muda mfupi baada ya barua ya Millya kusambaa kuwa amejizulu, Lema amesema hajashtuka wala kushangazwa na uamuzi huo wa kuamua kurejea CCM.

“Millya alikuwa ameshahama muda mrefu Chadema, ukiangalia matendo, mienendo yake, sisi tulishamwona amehama,” amesema.

Lema ambaye amekiri ni rafiki wa Millya na alihusika katika kumpokea wakati akihamia Chadema mwaka 2013 amesema, “Kilichonishangaza ni Millya kuchelewa kwenda CCM. Millya alipaswa kuwa mtu wa kwanza kabla ya madiwani na wabunge kuhamia lakini amekuwa wa mwisho ndicho kinanishangaza.”

“Bado sijaelewa hao wanaosema wanakwenda kuunga mkono, utaungaje mkono juhudi kukiwa na matatizo mengi, demokrasia inafinyangwa, waandishi wanatekwa, watu wanapotea, uchumi mgumu, ajira ni tatizo,” alihoji Lema.

“Unapokuwa mwanasiasa wa upinzani unapaswa kujua unapigania si masilahi yako bali ya wajukuu na vizazi vijavyo lakini kwa Millya ameamua kujinufaisha yeye binafsi,” amesema.