VIDEO:Lugola ambana IGP kuhusu alipo mbwa wa bandari

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akimweleza jambo mmoja wa askari wa kikosi cha mbwa kilichopo bandari ya Dar es Salaam wakati alipofanya ziara leo.

Muktasari:

Ampa hadi saa 12 awe amempa maelezo alipo mbwa huyo  aitwaye Hobby

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema ifikapo saa 12 jioni leo atahitaji maelezo kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro kuhusu alipo mbwa maalumu wa polisi wa kikosi cha Bandari ambaye hajulikani alipo.

Lugola ametoa kauli hiyo leo, Alhamisi Julai 19, 2018 wakati alipofanya ziara Bandari ya Dar es Salaam, kwa ajili ya kuona utendaji kazi wa jeshi la polisi bandarini hapo.

Amesema kikosi kina jumla ya mbwa sita maalumu, wawili wapo mafunzoni na wanabaki wanne ambapo kati yao mmoja aitwaye Hobby hajulikani alipo.

Alisema ameulizia alipo mbwa huyo lakini haijulikani alipopelekwa wala alipolala tangu alivyoondolewa jana asubuhi.

“Taarifa nilizonazo matumizi ya mbwa hawa siyo mazuri baadhi wanachukuliwa na kukodishwa kwa ajili ya kufanya shughuli nyingine. Nimesikitishwa na kitendo hiki na maelezo niliyopewa hajaniridhishwa kwa sababu mbwa hawa kwetu ni askari,”

“ Nikimaliza ziara yangu leo saa 12 jioni IGP (Sirro) yeye mwenyewe anipigie simu akiwa na huyu mbwa  pale polisi Bandari ili niweze kujiridhisha alikuwa wapi na alikwenda kufanya nini.” amesema Lugola.

 Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Mwibara amesema mbwa hao wana uwezo wa aina mbalimbali ikiwamo kunusa silaha, pembe za ndovu na dawa za kulevya zinazoingia au kusafarishwa kwa kutumia bandari hiyo.