Mafuriko yaua wawili Arusha

Gari likiwa limetumbukia katika daraja eneo la Sanawari jijini Arusha

Muktasari:

  • Hadi jana watu wawili wameripotiwa kufariki dunia na zaidi ya nyumba 50 na miundombinu kadhaa kuharibiwa.

Arusha. Wakazi wa Mkoa wa Arusha, wametakiwa kuchukuwa tahadhari, kutokana na mvua ambazo zinaendelea kunyesha na kusababisha madhara katika maeneo mbalimbali.

Hadi jana watu wawili wameripotiwa kufariki dunia na zaidi ya nyumba 50 na miundombinu kadhaa kuharibiwa.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Yusuph Ilembo amesema kutokana na mvua ambazo zinanyesha ni muhimu watu kuchukua tahadhari.

Amesema hata hivyo, matukio mengi  ya athari za mvua hizo hayajaripotiwa polisi hivyo, akatoa wito wananchi kutoa taarifa polisi  kwa viongozi wa vijiji na mitaa wanapokabiliwa na madhara ya mvua.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Idd Kimanta aliyekuwa akikagua athari za mvua katika maeneo la Nduruma, Bulka na Mushono amesema mvua zimesababisha madhara makubwa.

"Tumeokota mwili wa mwanamke mmoja katika eneo la Mushono hata hivyo inaonekana amefariki baada ya kubebwa na mafuriko mbali na eneo hili,"amesema

Katika jiji la Arusha, Maeneo ya Kata ya Murieti, Unga Limited, Sakina, Mushono na Mianzini, mvua zimesababisha uharibifu mkubwa wa nyumba za watu na kuharibu miondombinu mbalimbali.

Katika Kata ya Muriet mvua imeleta madhara ikiwamo kuharibika kwa miundombinu ya barabara na kusababisha magari ya abiria kukwama kuendelea na safari.