Magufuli amtumbua bosi wa Dart, abatilisha uamuzi dakika 10 baadaye
Muktasari:
Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo amezungumza na waandishi wa habari akieleza uamuzi aliouchukua Rais Magufuli wa kutengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Dart, Ronald Lwakatale lakini dakika 10 baadaye akabatilisha uamuzi huo
Dodoma. Rais John Magufuli ametengua nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Mabasi ya Mwendokasi (Dart), Ronald Lwakatale na kumteua Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) Mkoa wa Singida, Leonard Kapongo lakini dakika 10 baadae akabatilisha uamuzi huo.
Hali hiyo ilijitokeza leo wakati Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alipowaambia waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu kutenguliwa kwa mkurugenzi huyo.
Alisema hata hivyo hivi karibuni kumekuwa na mdororo mkubwa na kwamba jambo hilo haliridhishi kabisa.
“Jambo hili katika ofisi yangu halitutiii amani kabisa. Kutokana na hilo Mheshimiwa Rais ambaye ni mwenye dhamana tawala za mikoa na Serikali za mitaa ameridhia kutenguliwa kwa mtendaji mkuu wa wakala huo Mhandisi Ronald Lwakatare na yeye atapangiwa kazi nyingine.” .
“Nafasi yake itachukuliwa na Mhandisi Leonard Kapongo ambaye ni Meneja wa Tanroad Mkoa wa Singida na uteuzi huo unaanza leo mara moja. Jukumu lake kubwa sasa atakwenda kuweka utaratibu mzuri wa kurudisha hali nzuri ya usafiri katika jiji la Dar es Salaam.”
Baada ya kumalizika kwa mkutano huo, waandishi waliondoka na walipofika getini walielezwa na walinzi kwamba wanaitwa tena na Waziri Jafo.
Mara baada ya kurejea, Jafo alizungumza tena na waandishi akisema kuna mabadiliko kuhusu taarifa hiyo kwamba mkurugenzi huyo aliyetumbuliwa ataendelea na shughuli zake kama kawaida ila anatakiwa kujitathimini.
“Na leo hii kama mmeshuhudia kuwa watu wengine wamepita katika madirisha na nikiwa kama Waziri wa Tamisemi siridhiki na mwenendo huu namuagiza mtendaji mkuu anipe taarifa nini kinachoendelea. Kwa nini kuna hali ya kusuasua?” alisema.
Alisema kumekuwa na malalamiko ya wafanyakazi kwa upande wa mtoa huduma (UDART) na kwamba wanapogoma watu wamekuwa wakijua wafanyakazi hao wako chini ya Dart lakini ukweli ni kwamba wako chini ya UDART.
“Yeye anapofanya mambo tofauti na matarajio maana yake anakwamisha usafiri. Namuagiza Lwakatare amsimamie kwa karibu huyu mtoa huduma na hatutaki kuona hali hii inaemndelea,” alisema.
Pia Jafo amemuagiza Naibu Waziri wake Joseph Kakunda kukutana na uongozi wa Dart pamoja UDART ili kujua nini kinachoendelea na kesho ampe taarifa jambo gani limebainika.
“Lakini pia namuagiza Katibu Mkuu (Tamisemi) aangalie kama kuna watendaji wa ngazi mbalimbali katika Dart ambao kwa njia moja ama nyingine wanashiriki kufanya hujuma wa mwenendo huu usio mzuri afanye mabadiliko haraka,” alisema.
Amemuagiza Lwakatare kufanya mchakato wa haraka wa manunuzi wa kupata mtoa huduma wa moja kwa moja kwasababu aliyepo ni wa kipindi cha mpito.