Majaliwa: Tanzania inaongoza kwa uwekezaji Afrika Mashariki

Muktasari:

Majaliwa alisema hayo jana alipokuwa akihutubia kongamano la biashara kati ya Tanzania na China kwenye Hoteli ya Winstin Beijing, China.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Tanzania inaongoza kwa kupokea uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Majaliwa alisema hayo jana alipokuwa akihutubia kongamano la biashara kati ya Tanzania na China kwenye Hoteli ya Winstin Beijing, China.

Taarifa iliyotolewa jana na ofisi ya Waziri Mkuu, ilimnukuu Majaliwa akisema Tanzania imethibitika ni Taifa lililodhamiria kwa dhati kujenga uchumi wa viwanda, pamoja na kulinda na kudumisha amani na utulivu.

“Mtiririko wa uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja nchini umeongezeka kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita na sasa wawekezaji wameipa kipaumbele Tanzania kama kitovu cha uwekezaji barani Afrika,” alisema Majaliwa.

Alisema ripoti ya uwekezaji duniani iliyotolewa mwaka 2018, inaonyesha Tanzania inaongoza kwa kupokea uwekezaji katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na imepokea kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.2 mwaka 2017.

Alisema Tanzania inafanya juhudi kubwa ili iweze kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, hivyo imeweka mkazo katika kujenga msingi imara wa viwanda.

“Ili kufanikisha hilo, tumeandaa ukanda wa kuzalisha kwa ajili ya mauzo ya nje na ukanda maalumu wa kiuchumi tukilenga kutimiza mkakakati wetu wa kukuza uchumi wa viwanda na biashara,” alisema Majaliwa.

Kuhusu sekta ya fedha, alisema Tanzania inawakaribisha wawekezaji kuanzisha taasisi za kifedha kama vile benki kwa ajili ya kutoa mikopo midogomidogo, benki za uwekezaji, benki za kilimo na za biashara.

Akizungumzia uwekezaji kutoka China uliosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kati ya Novemba 2015 hadi Oktoba 2017, Waziri Mkuu alisema umefikia thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.077 na umejikita katika meneo ya kilimo, majengo ya biashara, rasilimali watu, viwanda na utalii.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema kuna fursa nyingi kwenye sekta ya huduma hususan katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ambayo ni miongoni mwa sekta ndogo zinazokuwa kwa haraka nchini Tanzania.

Pia, kumekuwa na ukuaji na mageuzi ya haraka katika soko la Tehama nchini kwa miaka 10 iliyopita. “Soko la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano limekuwa kwa ongezeko la watumiaji, aina ya huduma zinazotolewa pamoja na kupanuka kwa eneo ambalo huduma hizo hutolewa.”

“Maeneo ya kuwekeza ni pamoja na utoaji wa huduma za simu hususan katika maeneo ya vijijini, utoaji na uendeshaji wa huduma za mtandao pamoja na ukarabati na matengenezo ya vifaa vya mawasiliano. Tunawakaribisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo haya.”

Alisema kwa wale ambao nia yao ni kuwekeza katika kilimo, Tanzania ina hekta milioni 44 za ardhi inayofaa kwa kilimo na takribani hekta milioni 29.4 kwa ajili ya umwagiliaji.

“Ninawakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika kilimo cha biashara kwa mazao kama miwa, mpunga, ngano, kahawa, chai na mahindi. Tuna fursa kubwa ya kuwekeza katika kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari.”