Majaliwa akatisha ziara yake Dodoma, aenda Ukerewe

Muktasari:

Waziri Mkuu Majaliwa leo Septemba 21,2018 amekatisha ziara yake jijini Dodoma aliyoianza jana ili kwenda kuwafariji wananchi waliopata maafa katika ajali ya MV Nyerere

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekatisha ziara ya Mkoa wa Dodoma na kwenda Ukerewe jijini Mwanza kuwafariji wananchi waliopatwa na maafa kutokana na ajali ya kivuko cha MV Nyerere.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa na ziara ya kikazi ya siku saba jijini Dodoma iliyoanza jana, ametangaza uamuzi huo leo mchana Ijumaa, Septemba 21, 2018 wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Chandama wilayani Chemba ambao walisimamisha msafara wake ili wamweleze kero kubwa ya maji inayowakabili.

“Nimelazimika kukatisha ziara yangu na wala sitakwenda Kwa Mtoro ili niende kuwafariji wenzetu waliopatwa na msiba wa kupoteza ndugu zao kutokana na ajali iliyotokea jana usiku,” amesema Majaliwa

“Idadi ya waliopoteza maisha imefikia 91 ni msiba mkubwa kwa Taifa letu,” ameongeza

Taarifa iliyotumwa na kitengo cha mawasiliano cha ofisi ya waziri mkuu kimesema Majaliwa alikuwa akitokea kijiji cha Itolwa kata ya Jangalo ambako alikuwa na mkutano wa hadhara ambako aliwaeleza wananchi wa vijiji vya Itolwa, Mapango na Chandama kwamba Serikali imetenga Sh5.6 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji kwenye wilaya hiyo.

Akijibu kero kuhusu ubovu wa barabara, Waziri Mkuu amesema amebaini ukubwa wa tatizo la barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 10.3 lakini imetengewa Sh833 milioni ambazo alisema hazitoshi.

“Mhandisi wa Tarura nenda ukakae na timu yako, inabidi mfanye upya mahesabu yenu kwa sababu barabara hii ni ndefu na ina madaraja mengi lakini pia inapita kwenye vijiji vingi. Wenzenu Kondoa wamepata Sh7 bilioni, sasa hii Sh800 milioni hata sijui itaanzia wapi,” amesema.

“Barabara hii inapita kwenye vijiji vingi vikubwa na wakazi wa huku ni wengi. Hata kama kwa sasa hatuwezi kuijenga kwa kiwango cha lami, inapaswa ijengwe vizuri kwa kiwango kinachoweza kupitika kwa mwaka mzima,” alisema.

Aliwasisitiza watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba waache tabia ya kupenda kukaa ofisini na badala yake waende vijijini ili wakawasikilize wananchi na kutatua kero zao.