‘Apps’ hizi si za kukosa kwa wanafunzi

Tuesday November 13 2018

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi

Kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia imeendelea kugusa kila kona, na sasa wanafunzi nao wanarahisishiwa maisha.

Kama wewe ni mwanafunzi wa shule ama chuo na una miliki simu ya kisasa, tabiti au kompyuta mpakato, usiishie kujaza miziki na app za mitandao ya kijamii. Zipo app muhimu ambazo zinaweza kukusaidia kwenye masomo yako.

Evernote

Ukiwa chuoni hakuna sababu ya kubeba mzigo wa vitabu na madaftari; hakikisha una mpangilio mzuri wa kuhifadhi ‘notes’.

Evernote ni app maalum kwa ajili ya kazi hiyo, inakuwezesha kuwa na akaunti maalum ambayo utaitumia picha, sauti, video na maandishi.

Ukiwa nayo app hii huna sababu ya kubeba daftari au notibuku kubwa muda wote, vitu vyako vya muhimu vitakuwa kwenye simu yako ya kiganjani.

Endapo nutibuku yako itapotea, usiumize kichwa kwa kuwa ‘nondo’ zitakuwa kwenye akaunti yako. Angalizo unapotumia app hii haina maana uache kuandika, inatakiwa uandike kwa kifupi kisha kwa upana zaidi uhifadhi humu.

Babylon

Unaposoma na kukutana na lugha mpya, kamusi ni kitu muhimu kuwa nacho ikusaidie kupata maana halisi ya neno ulilokutana nalo.

Ukishakuwa na simu ya kisasa ya mkononi, unachopaswa ni kupakua App ya Babylon iwe mwongozo wako.

App hii ina maneno na maana zake ya lugha 75 . Pale utakapokutana na neno usilolielewa kutoka lugha ya kigeni, tumia app hii kukuletea maana kwa lugha rahisi unayoifahamu.

Dragon Dictation

Inapotokea huwezi kuandika kwa haraka kitu ulichojifunza au kukisikia app ya Dragon Dictation ndio msaada kwa wakati huo.

Hii inakupa fursa ya kuongea na yenyewe ikaandika kile unachokisema kwa haraka zaidi, kisha ukapitia na kusoma utakapopata wasaa mzuri. Kupitia app hii unaweza kuandika insha kwa kusema kile unachotaka kuandika na yenyewe ikasikiliza na kuandika kama utakavyotaka iwe.

Angalizo :App hii haikufanyii kazi zako kwa kuielekeza bali inasikiliza kile unachokitamka na kukiandika kama kilivyo.

Studious

Imewahi kukutokea umeingia darasani halafu ukasahau kutoa sauti kwenye simu yako na matokeo yake ikapiga kelele inapoita. Kama una tatizo hilo, app ya studious inakufaa. App hii inakuelekeza kuweka ratiba za vipindi vyako vya darasani ili iweze kufanya kazi. Baada ya hapo app itakuwa na uwezo wa kuondoa sauti ya simu yako kila utakapokuwa darasani.

Engineering Pro

Kama unachukua kozi ya uhandisi app hii ni muhimu kuwa nayo. Inawahusu wanaosoma kozi za umeme, kemia, na uhandisi wa mazingira. Ndani yake kuna zaidi ya formula 650 kwa ajili ya wanafunzi.

Skype

Wengi wanaweza kuwa wanaifahamu app hii lakini changamoto inakuja namna wanavyoitumia.

Kwa mwanachuo hasa anayesoma mbali na nyumbani, anaweza kuitumia hii kufanya mawasiliano na familia yake, rafiki zake na watu wake wa muhimu.

App hii pia inaweza kutumika kufanya usaili. Inaweza kutokea ukaomba nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo au kujitolea kwenye kampuni fulani na ukapewa maelekezo ya kufanya usaili kwa njia ya video. Inapotokea hivyo app hii ni sahihi zaidi.

Advertisement