Hii ndiyo faida ya kunyoosha viungo

Mazoezi ya kunyoosha mwili ni muhimu kwa ajili ya kukabiliana na hali yoyote inayojitokeza, mijongeo ya kimwili na kuzuia majeraha ya mwili.

Zoezi hili linahitajika kuwa sehemu ya maisha ya kila siku kwa mwanamichezo au yeyote anayefanya mazoezi kwa afya.

Zoezi la kunyoosha viungo huwezesha misuli ya mwili kupata utulivu na kuwezesha damu na virutubisho muhimu kutiririka kwa wingi katika mifupa plastiki (cartilage) na misuli.

Leo nitawapa dondoo tano za awali za faida za kiafya za zoezi la kunyooosha misuli ya mwili.

Faida ya kiafya ya kwanza ni kuondokana na uchovu hivyo kukufanya kupata utulivu wa kimwili na kiakili.

Kurundikana kwa shinikizo katika misuli huifanya misuli ya mwili kujikunyata, hivyo kuleta hali ya hisia za kukakamaa na kutohisi wepesi. Hali hii huleta madhara hasi kiakili pamoja na kimwili.

Mazoezi ya kunyoosha viungo vya mwili yana uwezo mkubwa wa kuondoa shinikizo lililopo katika misuli pindi unapoyafanya wakati kuamka huwezesha mwili na akili kuianza siku vizuri.

Kumbuka kuwa unapoamka na uchovu au kuumwa viungo huweza kukupa hofu pengine unaumwa na magonjwa ikiwamo malaria.

Mazoezi haya yanaifanya misuli ya mwili isibane na kuipa utulivu hivyo kutoa nafasi kwa damu kutiririka kirahisi.

Pia, mazoezi haya husababisha mwili kutiririsha kemikali mwili ijulikanayo kama Endorphins inayoufanya mwili kupata hisia za furaha.

Vile vile kufanya mazoezi haya kabla ya kwenda kulala husaidia kukupa usingizi mzuri.

Faida ya pili ni kusaidia kuweka ulalo sahihi wa mwili, kwa kunyoosha misuli ya mwili iliyokakamaa husaidia kuivuta na kuirudisha katika sehemu yake asilia inayotakiwa kuwapo.

Kunyoosha misuli kama ya eneo la chini mgongoni, kifuani na mabega husaidia kuuweka uti wa mgongo katika mpangilio sahihi hivyo kuboresha mkao wake.

Mkao sahihi wa mgongo huepusha uchovu na maumivu.

Faida ya tatu kiafya ni kuimarisha wepesi wa mwili (flexibility), wepesi huufanya mwili kuwa na utayari wa mabadiliko wakati wowote ikiwamo mijongeo mbalimbali kama kuruka, kukimbia au kujipinda bila tatizo. Wepesi wa mwili kwa mijongeo hii huupunguzia mwili kazi kubwa, kwa kuwa mwili utatumia nguvu kidogo kwasababu viungo kama maungio na misuli vinakuwa na wepesi kiutendaji.

Vile vile wepesi husaidia kuboresha utendaji wa kimwili na kupunguza hatari ya kupata majeraha ya mara kwa mara wakati wa michezo.

Faida ya nne ni kuongeza uwezo (stamina), kwa kunyoosha viungo vya mwili huifanya misuli kuwa laini na myepesi hivyo kuondokana na kukamaa na uchovu . Hii ni kwa sababu damu hutiririka kwa wingi maeneo hayo.

Kadiri unavyofanya mazoezi ndivyo pia mwili huchoma kiasi kikubwa cha nishati (glucose).

Kufanya zoezi hili husaidia kuchelewesha kujijenga kwa uchovu wa mwili kwa kusaidia damu yenye oksijeni kufika kwa wingi katika misuli, hivyo kuongeza utimamu wa mwili.

Faida ya tano ni kupunguza hatari ya kupata majeraha, kitendo cha zoezi hili kuifanya misuli kupokea damu na virutubisho kwa wingi huwa na faida kubwa kiafya kwani hupunguza vijidonda vya misuli na vile vile husaidia majeraha ya misuli na maungio kupona kwa haraka.

Mwandishi wa makala haya ni daktari wa binadamu