Je, ni lazima kuku kukatwa mdomo?

Muktasari:

Makala yaliyopita yalitoa mwongozo wa kuzingatia uchambuzi wa kuanzisha miradi ya ufugaji mapema kabla mfugaji hajaanza ufugaji ili kuwa na uhakika wa kufanikiwa.

Tukikumbuka hapo awali mada ya kukata mdomo kuku iliwahi kujitokeza katika mfululizo wa makala hizi.

Makala yaliyopita yalitoa mwongozo wa kuzingatia uchambuzi wa kuanzisha miradi ya ufugaji mapema kabla mfugaji hajaanza ufugaji ili kuwa na uhakika wa kufanikiwa.

Makala haya ya leo ni muunganiko wa hatua za kuboresha miradi yetu, hivyo sina budi tena kujadili kwa kina juu ya sababu za kukata mdomo ya kuku na aina nyinginezo za ndege wafugwao.

Kwanza kabla ya kuingia kwenye ufafanuzi, napenda kujibu swali hilo hapo juu kuwa: sio lazima kukata kuku mdomo!

Pengine inaweza kuwa sio kitu cha wazi kwa baadhi ya wasomaji au wafugaji kwamba kuku anakatwa mdomo kwa sababu gani na atakula vipi akikatwa mdomo wake. Maswali haya ni ya msingi kujiuliza ili upate sababu za kumkata au kutomkata mdomo kuku wako.

Kimsingi, mdomo wa kuku una asili ya ncha ambayo inaweza kukatwa kiasi kupunguza ncha kali yenye madhara ya kutoboa au kurarua na kujeruhi na kuku akaendelea na maisha kama kawaida. Kwa hiyo maana halisi ya kukata mdomo ni kuondoa incha kali ya mdomo.

Madhara ya kukata mdomo

Yapo madhara ambayo kuku anaweza kuyapata wakati wa kukatwa mdomo, ikiwamo kuvuja damu, kushindwa kula au kula kwa shida na kufa endapo amekatwa vibaya na ulimi ukakatika. Kwa kuku wenye umri mdogo hupata mshtuko sana hasa wanapokatwa na kuondolewa sehemu kubwa ya mdomo. Kuku wenye umri wa kutaga wanaweza kupunguza mayai kwa muda kutokana na mshtuko na kupunguza ulaji.

Mbali na madhara hayo ya kukata kuku mdomo wafugaji hulazimika kukata mdomo ya kuku, kutokana na madhara ya upande wa pili kuku asipokatwa mdomo.

Mara nyingi mdomo wa kuku unatumika kwa chakula lakini pia kuku hutumia mdomo wake kujihami, kupigana na kujeruhi wenzake. Hivyo kukatwa mdomo kwa kuku kumelenga kumfanya kuku asijeruhi wenzake au kutoboa mayai na kuyala. Kuku wasipokatwa mdomo ni jambo la kawaida kuona wakimshambulia mwenzao kwa kumtoboa toboa vidonda hadi kufa. Mfugaji anaweza kupoteza kuku wengi asipochukua hatua mapema.

Kwa hiyo moja kati ya hatua za kiusimamizi wa miradi ya kuku ni pamoja na kuhakikisha kuku hawauani wao kwa wao kwa kudonoana. Zingatia kanuni bora za ufaji kwa kujua mahitaji ya kuku na tahadhari za mapema zichukuliwe kulingana na umri na aina ya kuku ulionao.

Yafuatayo ni mambo yanayosababisha kuku kudonoana

Kwanza, kuchanganya kuku wenye rika tofauti kwenye banda moja au kuingiza kuku wageni kwenye banda la kuku wenyeji.

Pili, Kukiwa na kitu cha ncha kali bandani na kikamjeruhi kuku mmoja akaanza kuvuja damu, wengine wakiona kidonda cha kuku aliyejeruhiwa kila kuku kwenye banda atatafuta namna ya kudonoa kwenye jeraha hadi kuku mwenye jeraha atakapokufa au kuondolewa bandani.

Tatu, kuweka kuku wengi kupita kiasi kwenye banda au chumba kimoja. Kila kuku atatafuta namna ya kujitawala apate nafasi kwa kumdonoa mwenzake aliyekaribu asogee mbali; matokeo yake inakuwa tabia ya kila kuku.

Nne, Joto kuwa juu kuliko kwaida kwenye banda,hufanya kuku kutafuta namna ya kupata hewa safi, hivyo ili kupunguza joto hudonoana.

Tano, mwanga mkali kupita kiasi bandani wakati wa usiku huumiza macho kuku. Ni vizuri kuwasha taa zenye mwanga wa kawaida kwa saa nne za ziada wakati wa usiku bila kuzidisha saa 16 za mwanga.

Sita, upungufu wa lishe kwenye chakula wanachopewa kama vile upungufu wa protini na madini ya sodiamu, kalsiamu na fosiforasi husababisha kuku kuwa na hamu ya kudonoa kila kitu ikiwemo wao wenyewe.

Saba, kuweka kuku wachache bandani pia inaweza kusababisha kudonoana kwa sabau wanajuana . Ni vizuri kuwa na kuku wengi kiasi cha kujichanganya bila kujuana.

Nane, kubadilisha chakula ghafla au kubadilisha mazingira waliyozoea.

Tisa, kuweka vitagio vichache kuliko idadi ya mitetea wanaotaga. Kwa kawaida kiota kimoja kinafaa kuku watano zaidi ya hapo kuku watakutana kwenye kiota wakati kwa kutaga na hivyo kupigana.

Kitendo cha kukata midomo ni kuweka tahadhari hata kama mabadilko hayo yakitokea kuku wasidonoane na kuuana. Kuku waliokatwa, midomo yao hubaki butu hawawezi kuuana kwa majeraha ya kutoboana au kula mayai.

Njia za kujikinga endapo umeona tatizo limetokea ni kurekebisha vitu vinavyosababisha ikiwemo kuwatenga kuku waliojeruhiwa, kurekebisha lishe kwenye chakula chao na kukata midomo yao mapema kabla hawajafikia umri wa kutaga.

Namna ya kukta mdomo

Umri mzuri kukata mdomo ni miezi miwili hadi mitatu ya umri wao. Pia kwa tahadhari ya kuvuja damu au kukata ulimi, tumia kifaa chenye moto kukata na kuunguza hapo hapo ili damu isitoke.

Kwenye kitu cha moto kuku hurudisha ulimi nyuma usiungue hivyo utakata bila kumkata ulimi wake. Pia unapokata toa ncha ya mbele kwenye midomo yote juu na chini isipishane kuku akashindwa kula vizuri.

Usikate sana hadi kwenye nyama za mdomo kwani kuku atashindwa kula kabisa au kufa kwa kidonda. Kumbuka mdomo una mishipa mingi inayoenda moja kwa moja kwenye ubongo hivyo atapata shida akikatwa ovyo.