NATOA HOJA : Kenya wameanza, sisi Amunike tumemfungia hotelini

Monday October 1 2018Ibrahim Bakari

Ibrahim Bakari 

By Ibrahim Bakari

Timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars ilicheza na Ghana katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Afrika 2019 kule Cameroon.

Katika mchezo huo, Kenya ilishinda bao 1-0 bila kuwa na nahodha wake, Victor Wanyama.

Wanyama anayekipiga, Tottenham Hotspurs hakuwepo kwa kuwa alikuwa ametoka kwenye kuuguza majeraha hivyo asingeweza kucheza.

Pamoja na kubakia London, ni kama ilimkera kocha wa Harambee, Sebastien Migne ambaye baadaye alisema hataki kudenguliwa na wachezaji. Atakuwa akiangalia wachezaji wenye moyo na wazalendo.

Hiyo aliungwa mkono na kocha wa Ghana, Kwesi Appiah ambaye naye alikumbana na kadhia ya kuwakosa akina Ayew.

Alisema hawezi kuwabembeleza wachezaji wanaoringa kwa kuwa kuna wachezaji wengi.

Kocha wa Kenya alisema kuwa alichokuwa anataka kwa Wanyama kuja nchini ni kuwapa motisha wachezaji wenzake kama nahodha na hata kama alikuwa hachezi.

Migne aliamini kwamba kama angekuja, wangepata morari zaidi.

Kwa Migne sasa, juzi juzi alikuwa London akiwa katika ziara ya kuzungukia na kuwaina wachezaji wake.

Akiwa London, alizungumza na Wanyama na kwanza alimweleza kwanini hakuja, lakini pia alimwambia yuko tayari kucheza mechi ya Ethiopia baadaye mwezi huu kwa kuwa ameshapona vizuri.

Migne katua London ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea wachezaji wake kujipanga kwa Afcon 2019.

Nilipoiona habari hii ya kutembelea wachezaji wao huko waliko wanakocheza soka, nikamkumbuka Emmanuel Amunike, kocha wetu wa Taifa Stars.

Juzi hapa kwenye mechi na Uganda aliita mapro tisa wakiongozwa na Mbwana Samatta.

Niliwahi kuandoka hapa kuwa inatakiwa ifike hatua wachezaji wanaitwa, na tunachoshuhudia ni ndege zikipishana kuleta wachezaji. Inapendeza sana kama ilivyo kwa wenzetu wa Afrika Magharibi na Kaskazini.

Anyway, hapa nataka kusema hii ya Migne. Ameanza kuzungukia wachezaji wake, sasa sisi Amunike tumemfungia hotelini badala ya kuspoti maeneo machache ya kuanza nayop akawaangalie wachezaji wetu.

Jarida hili la Spoti Mikiki linawasiliana na wachezaji wengi wa Tanzania kila siku na wengine wako hadi ligi za Brazil huko, mwingine yuko Chile, Qatar, Ukraine, Iceland, Marekani, Ureno ukiacha na hao ambao tayari wanaitwa. Mfano Ureno kuna Watanzania wawili wanacheza Ligi Daraja la Kwanza, wangetufaa hawa. Austria kule kuna dogo anaitwa Michael Lema amepandishwa Ligi Kuu ya nchi hiyo, Amunike angeenda kumuona.

Wengi wa wachezaji wana miaka 18 hadi 24, na ndio wenye damu inayochemka. Katika Fainali za Kombe la Dunia, wastani wa umri ulikuwa miaka 22 hadi 25 na hao wa U-20 akina Kylian Mbappe walikuwepo wa kutosha, lakini sisi tunabakia na wazee ambao kasi yao haiwezi kuendana na ulimwengu mpya wa vijana.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika, CAF, Tanzania imepangwa Kundi L pamoja na Uganda, Cape Verde na Lesotho.

Tumedroo mechi mbili, Lesotho na Uganda sasa kama tunataka kufika mbali, wachezaji wanaocheza nje ni muhimu wakichanganywa na wa ndani. Tusimfungie Amunike hotelini au kuishia mechi za ligi, aende akawaangalkie nini wanafanya huko duniani.

Advertisement