Kilimo cha mbogamboga ndio mpango wa mjini

“Nimezaliwa kwenye familia ya wafugaji. Hadi namaliza shahada wazazi wangu wamenisomesha kwa kufuga nguruwe na kuku hivyo haikuwa ngumu kwangu kufuata nyayo zao,”

 

BY Aurea Simtowe, Mwananchi asimtowe@mwananchi.co.tz

IN SUMMARY

  • Ni maneno ya Obison Obadia (29) ambaye ni ofisa masoko wa kampuni ya British American Tobacco ambaye ameamua kutafuta kipato cha ziada kwenye kilimo na ufugaji kujiletea maendeleo anayohitaji.

Advertisement

“Nimezaliwa kwenye familia ya wafugaji. Hadi namaliza shahada wazazi wangu wamenisomesha kwa kufuga nguruwe na kuku hivyo haikuwa ngumu kwangu kufuata nyayo zao,”

Ni maneno ya Obison Obadia (29) ambaye ni ofisa masoko wa kampuni ya British American Tobacco ambaye ameamua kutafuta kipato cha ziada kwenye kilimo na ufugaji kujiletea maendeleo anayohitaji.

“Mbali na kufuga najihushughulisha na kilimo cha mbogamboga kama vile bamia, nyanya chungu na matikiti maji ambayo ni ya muda mfupi. Najiongezea kipato nje ya mshahara,” anasema.

Obadia anasema alianza kulima Oktoba 2013 akiwa na mtaji wa Sh3 milioni. Aliuelekeza mtaji wake kwenye kilimo cha bamia na matikiti maji ambayo yalikuwa na soko kubwa wakati huo.

Alilima eka tatu na baada ya kuvuna kwa mara ya kwanza anasema alipata faida mara mbili ya kile alichowekeza suala lililomtia moyo wa kuendelea kulima zaidi.

Kutokana na mafanikio hayo ya awali katika uwekezaji wake, anasema aliongeza mazao anayolima kulingana na mabadiliko ya msimu na mahitaji ya soko kuhakikisha anakuwa na bidhaa inayompa faida kila wakati.

“Kukiwa na mahitaji makubwa ya bamia basi nalima hizo kwa wingi na ikiwa ni mbogamboga nahamia huko pia vivyo hivyo kwa nyanya chungu na matikiti maji,” anasema Obadia.

Kutokana na mabadiliko ya uzalishaji anayoyafanya, anasema amekuwa na uhakika wa kuingiza hadi Sh2 milioni kwa mwezi kutokana na kilimo anachokifanya peke yake.

Mara nyingi huwa analima mbogamboga na bamia kutokana na uhitaji wake sokoni kutokuwa na msimu na urahisi wa ulimaji wake.

Wakati anaanza kilimo cha mazao hayo, anakumbuka masoko ya bidhaa zake yalikuwa changamoto jambo ambalo lilimlazimu kutumia elimu yake kwa ufasaha kuhakikisha anapata soko la uhakika.

“Baada ya kupata masoko sasa nikawa nawasaidia na wakulima wenzangu kuuza mazao yao huku wakinilipa kwa kila muamala ninaoufanikisha,” anasema Obadia.

Kwa uzoefu alionao, anasema kuna mahitaji makubwa ya mboga kiasi kwamba kuna wakati Dar es Salaam hutegemea zinatoka Chalinze, Bagamoyo, Morogoro na wakati mwingine jijini Dodoma.

“Licha ya ukubwa wa soko la ndani, nina mpango wa kutafuta soko la nje kwa kuungana na mtandao na watu au taasisi zinazosafirisha bidhaa za kilimo kwenda nje. Tayari nimeanza kutafuta vifungashio nitakavyovitumia,” anasema.

Mbali na kilimo, kwa kushirikiana na wenzake Obadia anatoa mafunzo ya kilimo cha mbogamboga kwa watu kwa mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

“Kwa wiki moja tunakuwa tunasoma nadharia na baadaye tunaenda shambani kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo yale tuliyoyasoma na kila mtu hulipia Sh15,000 kujifunza,” anasema Obadia.

Obadia anasema moja ya malengo yake ni kufikia uwezo wa kulima eka 100 kutoka nane anazolima sasa ili aweze kuuza bidhaa zake ndani na nje ya nchi.

More From Mwananchi
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept