Kwa nini sekta binafsi ni muhimu kulinda uchumi

Muktasari:

  • Uchumi wa nchi unaitegemea sekta binafsi kufanikisha mambo mengi. Uimara wa sekta binafsi unaathiriwa na na ukubwa wa sekta rasmi na isiyo rasmi. Kadri sekta rasmi inavyokuwa kubwa na imara ndivyo uchumi kwa ujumla wake unavyotengamaa.

Mjadala na utafiti kuhusu sekta isiyo rasmi nchini na kwingineko ni mpana ikijumuisha maana ya sekta isiyo rasmi, waliopo katika sekta hiyo na sababu za kuwapo kwao, faida na hasara za kuwa katika sekta hii na urasimishaji wake.

Kinachovutia zaidi katika mjadala huu ni kama kuna haja na ulazima wa kuirasimisha na endapo kuna haja ya kufanya hivyo, mchakato wake ufanyweje na nani atekeleze majukumu hayo.

Kuna maelezo mengi na tofauti kuhusu maana ya sekta isiyo rasmi. Wapo wanaosema hii ni sekta ambayo waliomo hawana sehemu rasmi ya kufanyia biashara, hawana leseni za biashara, hawana vitambulisho vya biashara na pengine hawalipi kodi ya mapato.

Vilevile hii ni sekta kubwa kwa maana ya idadi ya watu wanaojipatia mkate wao wa kila siku. Baadhi ya maelezo haya yanaweza kuwa na ukweli ilhali hayana ukweli. Baadhi ni maelezo yanayopatikana katika sekta rasmi pia.

Urasmi wa biashara ni zaidi ya kuwa na eneo maalumu la biashara, kuwa na leseni, kitambulisho na kulipa kodi. Kwa mfano, vitambulisho vya wamachinga vilivyoendelea kutolewa havimfanyi mfanyabiashara wa sekta isiyo rasmi kuhitimu na kuwa rasmi mara moja.

Urasmi wa biashara ni suala linahusisha mifumo kadhaa ya utendaji katika uratibu na uendeshaji wake. Urasimishaji unapaswa kuwa mchakato sio tukio la mara moja ili kuweka mifumo imara ya biashara itakayosimamiwa.

Ni juu ya kuwa na mifumo madhubuti ya uajiri, saa za kazi, mapumziko na vitu vingine muhimu katika uendeshaji biashara. Urasimishaji unahusu kufuata sheria, sera na miongozo ya biashara husika. Urasimishaji haupaswi kulazimishwa wala kufanywa kwa njia ya adhabu.

Biashara inapokuwa katika hali ya kutoweza kuendelea, inapojirasimisha huwa bora kuliko iliyolazimishwa kurasimishwa. Hata hivyo ni lazima kuweka vivutio ili kushawishi biashara kujirasimisha kwa hiyari bila shuruti.

Kuna mawazo yasiyo sahihi kuwa biashara kuwa rasmi ni suala la kuwa na karatasi zinaotolewa na mamlaka za usidhibiti na usimamizi. Kuwa na karatasi mfano leseni au utambulisho wa mlipa kodi ni muhimu lakini hakutoshelezi kuifanya biashara kuwa rasmi. Urasmi ni zaidi ya kuwa na karatasi hizo zinazohitajika na mamlaka za kisheria, kisera na kiudhibiti.

Urasimishaji

Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kuwa na biashara zilizo rasmi na mapato ya Serikali. Ndiyo maana katika bajeti ya Serikali mara nyingi katika kipengele cha sera za mapato sekta isiyo rasmi inatajwa.

Serikali inatambua mchango wa sekta isiyo rasmi na maeneo mengine muhimu ya uchumi ndio maana, wakati wote huweka mipango na mikakati ya kuhakikisha fursa zilizopo zinatumika ipasavyo kuchangia Hazina kuu ya Taifa.

Waziri wa fedha na mipango huzungumzia urasimishaji wa sekta isiyo rasmi kama miongoni mwa njia za kupanua wigo wa kodi ambao ni mwembamba. Hii ni kwa sababu biashara inaporasmishwa huonekana na kutambulika kiurahisi na mamlaka.

Hii hurahisisha kuingizwa katika wigo wa kodi. Mchakato wa urasimishaji na matokeo yake huzalisha mapato kwa Serikali. Leseni, vibali na tozo ni vyanzo vya mapato ya Serikali.

Kodi

Kati ya masuala ya kimjadala na utafiti kuhusu sekta isiyo rasmi ni kodi. Ni muhimu kufahamu endapo sekta hii inalipa au hailipi kodi na kama hailipi kuna haja ya kubadilisha hali hiyo. Kama ulazima huo upo basi kinachopaswa kufanyika kinahitaji kufafanuliwa.

Waliopo katika sekta hii wanalipa baadhi ya kodi. Kwa mfano wanalipa kodi za ulaji kama ya ongezeko la thamani ambayo ni asilimia 18. Hata hivyo kuna kodi mbalimbali ambazo baadhi hawalipi ambazo ni pamoja na kodi ya mapato, kodi ya ajira au kodi ya kuendeleza ujuzi.

Hata hivyo, kunapokuwapo utaratibu mzuri, sekta hii huweza kukadiriwa na kulipa kiasi fulani cha kodi. Kwa ukubwa wa sekta hii, ni fursa inayopotea kama wahusika hawatalipa kodi zinazolipwa na wafanyabiashara wa sekta rasmi.