Leo umekula, kesho itakuwaje?

Saturday June 30 2018GASTON NUNDUMA

GASTON NUNDUMA 

By Gaston Nunduma

Inasemekana kuwa Wazaramo na Wasambaa walitokea kwa mzazi mmoja. Katika kutafuta maisha Mzaramo alielekea Mkoa wa Pwani na Msambaa akaelekea kwenye milima ya Usambara. Mzazi wao alipoulizwa kuhusu walipo wanawe alisema, “mkubwa amekwenda kuzarama baharini na mdogo kaenda kusambara.”

Ni kawaida kwa watu kuwapa majina watoto kulingana na matukio makubwa yanayotukia wakati wa ujauzito wa mama zao. Huku Uswahilini wapo watoto wanaoitwa Mateso, Nifanyeje, Sina Sudi, Waseme na kadhalika kulingana na shida alizopata mama kutoka kwa jirani zake.

Ninaye jirani aliyeamua kumwita mwanaye “Hikinini”. Niliambiwa kuwa watu walikuwa wakimsimanga Mama Hiki hata kufikia kumuita tasa alipochelewa kupata ujauzito. Alipoupata akawauliza “kama mimi ni tasa hiki ni nini?”

Vilevile si ajabu hata kiduchu kuwasikia wenzetu walio kwenye dunia ya kwanza wanapowaita watoto wao majina kama hayo kwa lugha zao.

Ukitafsiri jina la George Walker Bush kwa Kiswahili unapata maana ya Mtembea Vichakani. Kumbuka pia enzi zile John Walker alibatizwa jina hilo kutokana na tabia yake ya kutembea kilomita 30 kutoka nyumbani hadi shamba, shamba hadi kilabuni na kisha kilabuni hadi nyumbani.

Tabia hizi zipo duniani kote kwa sababu wazazi ni walewale wanaozaa watoto walewale. Watoto hufunzwa kwa tamaduni za kwao na wakikua huchangamana, kuoana na hata kuzaa pamoja. Wanaijenga dunia yao waliyoirithi kutoka kwa mababu na wahenga wao.

Kama vile Wazarama na Wasambara, binadamu wote hujiongeza kwa elimu. Kutembea ni nyenzo kubwa kwenye kuitafuta elimu. Ramadhani Mtoro Ongara (marehemu) aliwahi kusema tembea ujionee, utajifunza tabia za watu na nchi zao. Aliongeza kuwa duniani kuna mengi ambayo yanakusubiri. Katika historia ya dunia unasoma safari za akina Livingstone, Vasco da Gama na wengineo. Tunaona jinsi walivyopanua akili zao hata wakamudu kutuongopea kuwa Afrika ilikuwa tupu. Waliweza hata kushikilia maeneo na kuyapa majina ya viongozi wao (akina Victoria), kisha kuwauzia ama kuwazawadia.

Walter Rodney aliandika kitabu kuelezea jinsi Ulaya inavyoshusha uchumi wa Afrika. Alisema iwapo Afrika itajiongeza na Mzungu kushindwa kumnyonya, basi ipo hatari ya Ulaya na Marekani kuwa wafagizi wa Waafrika. Alitoa mifano ya tofauti za rasilimali baina ya Afrika na Ulaya.

Kwa hiyo ili wao waendelee kuwa matajiri ni lazima watutawale kiuchumi na kiakili. Hii ndiyo maana Mfalme Haile Selassie alipotaka uwepo ulinganifu wa elimu baina yao na sisi, waligoma. Nasikia pia ilikuwa ndiyo sababu ya uharibifu wa Chuo Kikuu cha Timbuktu nchini Mali. Mwaka 1976 baada ya kifo cha Mao, Wachina walitetereka kidogo kwani walikuwa wakiendeshwa na sera za Mao kwenye kila kitu. Lakini alipoingia Hua Guofeng aliendeleza sera za kupambana na demokrasia na ubepari kwa nguvu zote hadi kuwatokomeza wapinzani waliosaidiwa na mabeberu.

Akaja Deng Xiaoping. Yeye baada ya kuona jinsi mabadiliko ya biashara na uchumi duniani, alilegeza kidogo misimamo. Alikubali kubadilishana uzoefu na mabepari kama Rais Jimmy Carter wa Marekani na Kim il-Sung wa Korea.

Lakini pia wakati huohuo Wachina walimwagwa kila kona ya dunia kujifunza mambo ya wenzao. Wakageuka kuwa wataalamu wa kazi kuanzia ufundi mpaka vibarua. Uwanja wa Taifa Dar es Salaam ulijengwa na wahandisi hadi wachanganya zege.

Hivi leo China inatishia kuuongoza uchumi wa dunia baada ya kuweka malengo muda mrefu. Kila kiongozi anayeingia anaendeleza alipoacha aliyemtangulia. Pamoja na makosa yaliyofanywa wakati wa ukomunisti, Wachina hawajauacha ukomunisti bali waliurekebisha kwa kupunguza kasoro.

Tanzania sasa inalenga kwenye uchumi wa viwanda. Ni jambo zuri na la msingi kwa kuwa hakuna maendeleo bila uzalishaji. Lakini bahati mbaya yetu ni kubadilisha mfumo kila awamu ya uongozi bila kuchota mazuri yaliyotangulia.

Mwalimu Julius Nyerere alikuja na Ujamaa na Kujitegemea. Akaweka misingi ya vijiji vya ujamaa, Azimio la Arusha, vyama vya ushirika na kadhalika. Kinadharia ilikuwa safi sana, ingawa kiutekelezaji ilikuwa na changamoto nyingi.

Hapa izingatiwe kuwa sina nia ya kukosoa tawala zilizopita, bali najaribu kufurahia mafanikio ya China baada ya kusimama kwenye malengo yao.

Pamoja na makosa ambayo pengine yalizorotesha uchumi wa Tanzania, haikuwa busara kuvunja kila msingi uliosimikwa. Hivi sasa badala ya kwenda mbele tunarudi kupambana na mafisadi. Tunaendelea kunyosheana vidole na walaji wa fedha, matumizi mabaya ya fedha za umma na kadhalika.

Bado nasisitiza kuwa kwa mwenendo huu hatutafika kwenye nchi ya uchumi wa viwanda. Roma haikujengwa kwa siku moja na bila shaka kiongozi anayesimamia uchumi wa viwanda atamaliza muda wake na kupokewa na kiongozi mwingine. Tusipokuwa kama Wachina, kila kiongozi mpya atakuja na mapya yake. Anayetangulia anaweza kujenga viwanda na kukusanya kodi lakini anayemfuatia anakuja kuzitawanya badala ya kuzielekeza katika maendeleo. Nchi itaendelea kuwa hoi na wananchi wake kubakia kuwa ni maskini.

Advertisement